Apple:Hakuna anayeweza kudukua iPhone

Haki miliki ya picha Thinkstock
Image caption Apple:imefichua hakuna anayeweza kudukua iPhone

Kampuni ya kutengeneza simu na bidhaa za kielektroniki kutoka Marekani, Apple, imefichua kuwa hakuna anayeweza kudukua siri za wateja wa simu za IPhone.

Katika stakabathi rasmi zilizowasilishwa mahakamani huko Marekani,kampuni hiyo inasema mfumo unaotumika kwa sasa wa iOS 8 hauwezi kudukuliwa.

hata kampuni yenyewe hainauwezo wa kudukua simu zinazotumia mfumo huo na bora zaidi.

Hii inamaanisha kuwa takriban asilimia 90% ya simu zake haziwezi kudukuliwa .

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Takriban asilimia 90% ya simu za Apple haziwezi kudukuliwa .

Mahakama hiyo ilikuwa imeomba Apple isaidie serikali kufungua simu ya mshukiwa mmoja iliyokamatwa kwa nia ya kupata taarifa muhimu.

Mwenye simu hiyo amekataa kata kata kuwapa maafisa wa polisi anuani ya kuifungua simu hiyo akidai ni ukiukaji wa haki zake za kimsingi.

Japo simu hiyo sio ya kisasa Apple imekataa kuifungua.

Kampuni hiyo yenye makao yake makuu huko California inasema kuwa endapo itashurutishwa kuifungua simu hiyo mamilioni ya wateja wake watahisi wamesalitiwa na hivyo huenda wakasusia bidhaa zao.

''Endapo mahakama hii itaishurutisha Apple kufungua siyo simu bila idhini ya mwenyewe imani ya mamilioni ya wateja wetu itatikiswa vibaya na huenda ikaathiri pakubwa mauzo na imani yao kwa bidhaa zetu''taarifa hiyo ya Apple ilisema.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Tim Cook amesema kuwa kampuni hiyo haitawaruhusu maafisa wa utawala wowote kudukua simu zao.

Hakimu mkuu katika mahakama ya Brooklyn New York James Orenstein ameratibu kikao kingine siku ya Alhamisi ilikujadili matukio na majibu hayo kutoka Apple.

Kwa mujibu wa Apple endapo serikali itapendekeza kuwa simu yeyote idukuliwe basi sharti mmiliki mwenyewe atoe anuani maalumu.

Wakati huohuo mkurugenzi mkuu wa Apple Tim Cook amesema kuwa kampuni hiyo haitawaruhusu maafisa wa utawala wowote kudukua simu zao.

Cook aliyasema hayo siku chache tu baada ya kuondoa takriban programu 250 kwenye soko la appstore zenye asili ya China zilizokuwa zinadukua anuani za siri za wamiliki wa simu.