Biden atangaza hatawania urais 2016

Biden Haki miliki ya picha AFP
Image caption Biden amesema hakuna muda wa kuandaa na kufanya kampeni ya kufana

Makamu wa Rais wa Marekani Joe Biden ametangaza kwamba hatawania urais mwaka ujao.

Ni wazi sasa kuwa Bernie Sanders ndiye mpinzani mkuu wa Mama Hillary Clinton kwa uwaniaji wa Urais wa Marekani kupitia chama cha Democrat, baada ya Makamu wa Rais Joe Biden kutangaza kuwa hatagombea Urais wa Marekani.

Akiongea katika mji mkuu wa New York, Bwana Sanders alimpongeza Makamu wa Rais kwa kutoa huduma muhimu kwa jamii kwa muda mrefu.

Biden amesema hataweza kujiingiza kwenye kinyang’anyiro cha kusaka tiketi ya chama cha Democratic kuwania urais uchaguzi mkuu wa 2016.

Kiongozi huyo amesema familia yake ilikuwa tayari baada ya kifo cha mwanawe wa kiume mapema mwaka huu, lakini sasa hana muda.

Aidha, amesema litakuwa kosa kubwa kwa mtu yeyote katika chama cha Democratic kutotambua rekodi nzuri ya Rais Barack Obama.

Wafuasi wa chama cha Democratic waliokuwa wakitaka mgombea mwingine badala ya Hillary Clinton wamekuwa wakimshinikiza mzee huyo wa miaka 72 kuwania.

Ingawa amesema kuwa hatawania, Bw Biden amesema hatakaa kimya.

“Ninakusudia kuzungumza na kueleza mambo waziwazi na kwa nguvu kuhusu msimamo wetu kama chama na kule tunakofaa kuelekea kama taifa.”

Alisema mgombea yeyote wa chama hicho atafanya “kosa kubwa” kutotambua mchango wa Obama.

Aidha, alitoa wito wa kusitishwa kwa siasa chafu na za kugawanya watu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Biden aliandamana na mkewe Jill na Rais Barack Obama

"Ninaamini lazima tusitishe siasa za mgawanyiko ambazo zinasambaratisha taifa letu,” alisema wakati wa kutoa tangazo hilo uwanja wa Rose Garden katika ikulu ya White House, akiandamana na mkewe Jill na Bw Obama.

Akirudia kumshutumu Clinton kwa mara nyingine, alisema ni kosa kuwatazama wafuasi wa chama cha Republican kama maadui.

Alipoulizwa wakati wa mdahalo wa wagombea urais wa chama cha Democratic, Bi Clinton alisema anajivunia kufanya uadui na wafuasi wa chama cha Republican.