‘Kijana wa saa’ kuhamia Qatar na familia yake

Ahmed Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ahmed alikutana na Rais Barack Obama Jumatatu

Kijana Mwislamu kutoka Texas Ahmed Mohamed, aliyehangaishwa baada ya mwalimu wake kudhani saa aliyokuwa amejitengenezea ilikuwa bomu, atahamia Qatar.

Ahmed, 14, amekubali ufadhili wa kimasomo kutoka kwa Wakfu wa Elimu na Sayansi wa Qatar, ambako ataenda kusomea.

Mvulana huyo alikutana na Rais Barack Obama katika ikulu ya White House Jumatatu.

Baada ya kuzuiliwa kwa muda kwa sababu ya saa, kisa chake kilivutia mamilioni ya watu na kujadiliwa sana mitandao ya kijamii.

Baadhi walidai alidhalilishwa kwa sababu ya jina lake na dini.

Maafisa wa serikali Irving Texas wametetea uamuzi wao, na kusema walikuwa tu wanajali usalama wa wanafunzi wengine.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Hii ndiyo saa aliyoitengeneza Ahmed

Wakfu huo wa Qatar utampa mvulana huyo ufadhili kamili wa elimu ya sekondari na chuo, kwa mujibu wa taarifa iliyotumwa kwa vyombo vya habari na wakfu huo.

"Familia yetu imeguswa sana na ukarimu na usaidizi ambao tumepata tangu kutokea kwa kisa hicho cha kukamatwa kwa Ahmed,” familia ya Ahmed ilisema kwenye taarifa hiyo.

"Kutoka White House hadi Sudan, hadi Mecca, tumekaribishwa na watu wa tabaka mbalimbali.”

Kwa mujibu wa familia yake, Ahmed atajiunga na mpango wa “Wavumbuzi Chipukizi” Wakfu wa Qatar na yeyea na familia yake yote watahamia Qatar.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ahmed alikutana na Rais Bashir mjini Khartoum

Wiki iliyopita, Ahmed alikutana na Rais wa Sudan Omar al-Bashir.