Wakulima Mbeya TZ:Kilimo hakitunufaishi

Image caption Wakulima Mbeya

Mkoa wa Mbeya ni moja ya mikoa inayotegemewa karibia na miji mingi mikubwa ya Tanzania katika uzalishaji wa chakula.

Mkoa huo ulioko Kusini Magharibi mwa Tanzania, una hali ya hewa inayoufanya kustawisha mazao mbalimbali ya chakula na biashara kama viazi, ndizi, chai, kahawa na mpunga.

Mkoa huo pia unaiunganisha Tanzania na nchi mbali mbali za kusini mwa Afrika hasa Zambia na hata kwa upande mwingine Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo

Image caption Wakulima kuamua kuhusu bei ya mazao yao Mbeya

Aidha miongoni mwa wanasiasa, mkoa huo ni moja ya mikoa muhimu kwa sababu ni mkoa wa tatu kwa kuwa na wapiga kura wengi baada ya Dar es Salaam na Mwanza.

Wapiga kura katika mkoa wa Mbeya pekee wanakadiriwa kufikia takribani milioni moja na laki tatu.

Pamoja na kuwa wakazi wa mkoa huo ni wakulima wazuri lakini wanasema hawajaneemeka na shughuli hiyo ya kilimo kama walivyomweleza mwandishi wa BBC Arnold Kayanda aliyeuzuru mkoa huo.

Image caption Taarifa ya wastani wa bei

Pamoja na wakazi wa mkoa huo kujishughulisha na kilimo, pia wanalalamika kuwa shughuli hiyo haiwafaidishi kutokana na sababu mbalimbali.

Sababu mojawapo inayotajwa na wakulima wa eneo la Ubaruku katika Wilaya ya Mbarali ni gharama kubwa za pembejeo.

Wanasema ni vigumu kununua mbolea kutokana na gharama ya juu ilihali wakishavuna soko siyo la uhakika.

Image caption Mavuno ya wakulima wa Mbeya Tanzania

Aidha wakulima hao wanadai kuwa siyo rahisi kwa mkulima wa kawaida kuweza kumudu kununua vifaa vya kilimo kama tinga dogo maarufu kama Power tiller kwa kuwa bei yake ni kubwa.

'Power tiller inauzwa milioni 12 na nusu, mimi nitaipata wapi hiyo? Na tukikopa fedha tunalazimika kuweka nyumba zetu kama dhamana kwa hivyo tunazipoteza nyumba zetu' anasema Mkulima wa Mpunga

Image caption Tingatinga Tanzania

Kutokana na kukosa soko la mazao yao ya kilimo, wakulima wa eneo la Igurusi wameamua kuanzisha soko lao linaloratibiwa na Muungano wa vikundi vya wakulima Tanzania MVIWATA.

Soko hili lina lengo la kuwapa nguvu wakulima ili kuamua bei ya kuuza mazao yao.