Mwanamke anayekabiliana na ugonjwa wa endometriosis

Millen Haki miliki ya picha Millen Magese
Image caption Magese amekataa kukata tamaa katika kukabiliana na endometriosis

Happiness Millen Magese ni shujaa wa kipekee kutoka Afrika. Si kwa sababu aliwahi kuwa Miss Tanzania au kwa sababu ni mlimbwende tajiri na maarufu duniani bali Millen Magese.

Ni shujaa wa kipekee kwa sababu amedhamiria kupambana na ugonjwa unaomdhoofisha kwa kuhamasisha mamilioni ya wanawake ambao maisha yao pia yameathirika na ugonjwa kama wake.

Yeye ni miongoni mwa wanawake wanaosumbuliwa na ugonjwa wa endometriosis. Endometriosis ni ugonjwa ambao huhusisha seli zinazofaa kuwa ndani ya mji wa uzazi kuwa nje ya mji huo.

Lakini licha ya uzito wa tatizo hilo amekuwa mkakamavu na kuweka bayana matatizo yake hayo, ambayo kwa wanawake wengi ingelikuwa ni siri ya mtungi.

Millen alipatikana na endometriosis miaka 13 baada yake kupata hedhi mara ya kwanza.

Ugonjwa huo tayari ulikuwa umekolea.

“Sikuwahi kufikiria kuwa siku yangu ya kwanza kuanza kupata hedhi ningeweza kuanza kupata maumivu makali ambayo yamekuwa ni vita vikali katika maisha yangu,” anaeleza.

Daktari Esther Eisenberg kutoka kituo cha kitaifa cha afya nchini Marekani anasema ugonjwa huo ambao husababisha ugumba kiini chake hakijulikani vyema.

“Inawezekana kuwa wakati mwanamke akiwa katika siku zake, ndipo madhara hujitokeza katika mishipa ya ukuta wa mji wa uzazi na damu hiyo ya hedhi kumwagika nje ya mishipa hiyo,” anasema.

Hivyo madhara yake huathiri maeneo yote ya mishipa ya uzazi yaani fallopian tubes, uteras na mji wote wa uzazi.

“Lakini ninachokiona hapa ni kwamba tunapaswa kufanya uchunguzi zaidi ili kuwa na uelewa mpana wa ugonjwa huu,” daktari huyo anatahadharisha.

Bi Magese amefanya jitihada kadhaa kuhakikisha anakabiliana na ugonjwa huu, hadi sasa amefanyiwa upasuaji mara 13 lakini mwenyewe anasema hajakata tamaa kutafuta tiba ya ugonjwa huo. Njia pekee kwa sasa huwa ni kufanyiwa upasuaji au kutumia homoni.

Lakini bado anatafuta mbinu nyingine ya kumsaidia kando na safari zake za hospitalini.

Maumivu yanapozidi sana, yeye hulazimika kunywa dawa za kupunguza maumivu na wakati mwingine hata kujidunga sindano.

Changamoto hizi zinazomkumba zimempea msukumo wa kuanzisha wakfu wa Millen Magese Foundation anaoutumia kuhamasisha uwepo na athari ya ugonjwa huu, ambao unaathiri wasichana wapatao milioni 176 kote duniani.

“Nilianzisha Millen Magese Foundation na mimi ni mshirika katika kampeni ya Let’s Face it < Period. Ni kampeni ambayo inatoa elimu kwa jamii kuhusiana na hedhi na usafi, suala ambalo kwangu mimi kila siku huwa najiuliza mwenyewe kama nilifanya jambo tofauti,” anasema Bi Magese.

"Huwa najiuliza, Niliwahi kutumia kitu gani kibaya au kwa nini ninapitia mateso haya kutokana na endometriosis? Na mwaka huu nimeanzisha kampeni inayosema Many Faces for Endo, Speak out!” (Sura nyingi za Endo, Usinyamaze).”

Haki miliki ya picha Millen Magese

Katika kampeni hiyo, wanawake hujipiga picha na kuwahamasisha wengine kuweka picha wakiwa kwenye pozi mbalimbali katika mtandao wa kijamii wa Instagram. Kampeni hiyo ilifana sana na ilinishindia tuzo.

Wakfu wa Millen Magese Foundation huhudumu nchini Marekani, Afrika Kusini na pia Tanzania.

Haki miliki ya picha

"Ninataka kuhamasisha watu kuhusu endometriosis na matatizo mengine yanayowakabili wanawake. Sitaki kuona msichana mwingine wa umri wa miaka 13 akiteseka kutokana na endometriosis.”