Watu 40 wafariki ajalini Ufaransa

Ajali Ufaransa Haki miliki ya picha
Image caption Ajali hiyo imetokea kusini magharibi mwa Ufaransa

Watu 40 waliokuwa wakienda kutalii wamefariki baada ya basi lao kugongana na lori katika barabara moja kusini magharibi mwa Ufaransa.

Ajali hiyo imetokea karibu na Puisseguin eneo la Gironde mashariki mwa Bordeaux, muda mfupi baada ya basi hilo kuanza safari kutoka mji ulio karibu.

Rais wa Ufaransa Francois Hollande ameandika kwenye Twitter kwamba serikali “imechukua hatua zote kushughulikia mkasa huo mbaya”.

Mkasa huo ndio mbaya zaidi kutokea barabarani Ufaransa tangu ajali iliyoua watu 52 mwaka 1982.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Ufaransa, ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa 07:30 saa za huko karibu na kijiji cha Puisseguin.

Magari yote mawili yaliwaka moto baada ya kugongana.

Abiria 41 walikuwa kwenye basi. Dereva wa lori alifariki. Ni watu wanane pekee walionusurika, watano wakiwa na majeraha.

Wengi wa waliokuwa kwenye basi hilo walitoka chama cha wazee kilicho katika mji wa Petit-Palais-et-Cornemps.

Kiini cha ajali hiyo bado hakijabainika.

Waziri mkuu wa Ufaransa Manuel Valls, pamoja na mawaziri wa masuala ya ndani na uchukuzi wanatarajiwa kutembelea eneo la mkasa.