Albino ashambuliwa pwani ya Tanzania

Albino Haki miliki ya picha Getty
Image caption Visa vya albino kushambuliwa na kukatwa viungo huongezeka sana wakati wa uchaguzi

Mwanamume mwenye ulemavu wa ngozi anauguza majeraha baada ya kushambuliwa na watu wasiojulikana eneo la Mkuranga, Tanzania.

Shambulio hilo dhidi ya albino huyo limetokea siku chache tu kabla ya uchaguzi mkuu kufanyika.

Kumekuwepo na wasiwasi kwamba huenda watu wenye ulemavu wakashambuliwa zaidi kwani baadhi ya watu wanaoamini katika ushirikina hudai viungo vyao vinaweza kumpa mtu bahati.

Wanaume watatu wanadaiwa kuingia kwa nguvu nyumbani kwa Mohammed Said, 35, katika mji huo ulio katika mwambao wa Pwani kilomita 42 kutoka mji mkuu wa kibiashara wa Dar es Salaam.

Walimkata kichwani kwa upanga wakati wa shambulio hilo Jumatano usiku.

Polisi wamesema wanawasaka watu hao.

Serikali mapema mwaka huu ilikiri kwamba huenda wanasiasa wanachochea hitaji kubwa la viungo vya binadamu kwani ripoti zilionyesha visa vya mashambulizi ya albino huongezeka wakati wa uchaguzi.

Januari mwaka huu, serikali ilipiga marufuku waganga wa kienyeji na takriban watu 200 wamekamatwa, mwandishi wa BBC Sammy Awami anasema.

Uchaguzi mkuu nchini Tanzania utafanyika Jumapili Oktoba 25.