Ameobi ajiunga na Bolton Wanderers

Ameobi Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ameobi alikaa muda mwingi Newscastle

Klabu inayocheza ligi ya daraja la pili nchini Uingereza Bolton Wanderers imemchukua mshambuliaji wa Nigeria Shola Ameobi kwa mkataba wa muda mfupi.

Mchezaji huyo aliyewahi kuchezea timu ya taifa ya Uingereza ya wachezaji wasioozidi umri wa miaka 21 aliwaridhisha wakati wa akifanyiwa majaribio katika klabu hiyo.

Mshambuliaji huyo wa miaka 34 alikaa muda wake mwingi Newcastle baada ya kukua kutoka akademi yao na alikaa kwa muda Stoke City kwa mkopo mwaka 2008.

Baada ya kuondoka Newcastle, alijiunga na klabu ya Uturuki Gaziantep BB. Miezi sita ya msimu uliopita alikaa Crystal Palace.

Alifunga mabao 11 katika mechi 21 akichezea Newcastle United kwenye ligi ya Championship mwaka 2009-10.

Ameobi, aliyechezea timu ya taifa ya Nigeria mechi 10, alikaa kwa muda mfupi mwezi Septemba mwaka huu katika klabu ya Wolves akifanyiwa majaribio, lakini baadaye akaondoka na kufanyiwa majaribio Bolton.

Klabu hiyo ya Bolton kwa sasa inashika mkia ligi hiyo ya daraja la pili baada ya kushinda mechi moja pekee msimu huu.