Israel na Jordan zaafikiana kuhusu Jerusalem

Kerry Haki miliki ya picha AFP
Image caption Kerry alikutana na Abbas Jumamosi mjini Amman

Israel na Jordan zimeafikiana kuhusu hatua ambazo zinalenga kumaliza uhasama ambao umekuwepo kuhusu moja ya maeneo matakatifu zaidi mjini Jerusalem, waziri wa mashauri ya kigeni wa Marekani John Kerry amesema.

Mzozo kuhusu eneo hilo umekuwa kiini cha machafuko mapya kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Bw Kerry alikuwa akizungumza baada ya mashauriano nchini Jordan, taifa linalotunza rasmi eneo ambalo kwa Wayahudi hujulikana kama Temple Mount lakini kwa Waislamu hujulikana kama Haram al-Sharif.

Amesema Israel imekariri tena ahadi ya kuendelea kuheshimu sheria zinazosimamia eneo hilo.

Kwenye machafuko ya hivi karibuni, Waisraeli wanane wameuawa na wengine kadha kujeruhiwa kwa kudungwa visu au kupigwa risasi na Wapalestina. Hii ni baada ya kutokea uvumi kwamba Israel ilipanga kubadilisha sheria zinazosimamia eneo hilo.

Haki miliki ya picha Reuters

Wapalestina karibu 50, baadhi wakiwa washambuliaji, wameuawa katika wiki za karibuni.

Bw Kerry, anayezuru eneo la Mashariki ya Kati, alikutana na kiongozi wa Wapalestina Mahmoud Abbas na Mfalme Abdullah wa Jordan mjini Amman Jumamosi.

"Ghasia hizi na uchochezi sharti vikome. Viongozi lazima waongoze katika hili,” Bw Kerry aliambia wanahabari.

Hatua alizotangaza za kurejesha amani eneo hilo ni pamoja na kufuatiliwa kwa matukio eneo hilo kila wakati kwa kutumia video na ahadi ya Israel kuheshimu Jordan kama mlinzi wa maeneo ya kihistoria ya eneo hilo.

Image caption Eneo la Temple Mount ni moja ya maeneo matakatifu zaidi kwa Wayahudi na Waislamu

Israel imesema haijapinga hali ya sasa kuhusu usimamizi wa Temple Mount na haina nia ya kufanya hivyo.