Morocco na Tunisia zafuzu kwa fainali za CHAN

Morocco Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ushindi wa Morocco dhidi ya Libya uliwezesha Tunisia kufuzu

Morocco walicharaza Libya 4-0 katika kanda ya Kaskazini ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Mabingwa wa Afrika kwa wachezaji wanaochezea barani (CHAN) za mwaka 2016 ambazo zitachezewa nchini Rwanda mwaka ujao.

Libya walihitaji kushinda mechi hiyo iliyochezwa Alhamisi ndipo wafuzu baada yao kushindwa 1-0 na Tunisia Jumatatu.

Morocco wanaongoza ligi hiyo ndogo ya timu tatu wakiwa na alama saba, Tunisia wakiwa wa pili na alama nne. Libya wanashika mkia na alama mbili.

Tunisia na Morocco zitakutaka kwenye mechi ya mwisho ya kanda hiyo Jumapili, Tunisia wakiwa nyumbani Rades.

Mabao ya Morocco dhidi ya Libya yalifungwa na Abdessalam Ben Jelloun, Abdessalad Lmobarakay, Rachid Housni na Mohammed Onajem.