Blair akiri huenda uvamizi Iraq ulichochea IS

Blair Haki miliki ya picha REUTERS
Image caption Blair alikuwa Waziri Mkuu wa Uingereza kuanzia 1997 hadi 2007

Tony Blair ameomba radhi kuhusiana na makosa yaliyofanyika katika Vita vya Iraq, na kusema kuna ukweli fulani kwamba vita hivyo vilichangia uwepo wa Islamic State.

Waziri mkuu huyo wa zamani wa Uingereza amesema “waliomuondoa madarakani Saddam" wanawajibika kwa kiasi fulani na hali ya sasa Iraq.

Lakini bado alitetea uvamizi uliotekelezwa na majeshi ya mataifa ya Magharibi, akisema ni vigumu “kuomba radhi” kwa kumtoa madarakani Saddam Hussein.

Amesema iwapo kiongozi huyo hangetimuliwa madarakani, Iraq huenda ingekuwa kama Syria leo.

Matamshi ya Bw Blair yamejiri muda mfupi kabla ya Sir John Chilcot kutangaza ratiba ya kukamilishwa kwa uchunguzi kuhusu vita hivyo.

Mwandishi wa BBC anayeshughulikia masuala ya siasa Iain Watson anasema ingawa Bw Blair ameomba msamaha, ni kwa mambo madogo sana.

Kwenye mahojiano na kituo cha runinga cha Marekani cha CNN, ambayo hayajapeperushwa, Bw Blair anasema hata ingawa sera zake Iraq hazikufanikiwa, waliofuata pia hawakufanikiwa.

Alidokeza kuwa iwapo mataifa ya Magharibi hayangeingilia kati Iraq, kuna uwezekano mkubwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yangelitokea, kama inavyofanyika sasa Syria.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Blair amekuwa akitetea uvamizi wa Iraq

Aliomba radhi kwa “baadhi ya makosa kwenye mipango” pamoja na “kosa la uelewa wetu kuhusu yale yangelifanyika baada ya kuondolewa kwa utawala wake”.

Lakini ameambia CNN kwamba iwapo angeulizwa iwapo “ingelikuwa vyema duniani” iwapo Saddam angelikuw abado madarakani, “Itanibidi kuachana na watu.”

Alipoulizwa iwapo kilichosababisha kuibuka kwa kundi la wapiganaji Islamic State (IS au ISIS), alijibu: “Ninadhani kuna ukweli fulani katika hilo.

"Bila shaka huwezi ukasema sisi tuliomuondoa madarakani Saddam mwaka 2003 hatuna lawama kutokana na hali sasa 2015, lakini ni muhimu kutambua kwamba wimbi la mageuzi mataifa ya Kiarabu mwaka 2011 labda pia yangeathiri Iraq leo.”