Uchaguzi mkuu waanza Ivory Coast

Ivory Coast Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wafuasi wa Ouattara wana imani atashinda

Uchaguzi mkuu umeanza nchini Ivory Coast, ukiwa wa kwanza baada mapigano ya wenyewe kwa wenyewe yaliyotokana na uchaguzi mwingine 2010.

Mapigano hayo yalimalizika 2011.

Wengi wa wagombea wa upinzani wamejiondoa kutoka kwenye kinyang’anyiro hicho wakidai uchaguzi huo hautakuwa huru na wa haki.

Rais Alassane Ouattara anawania akitaka kuongoza kwa muhula wa pili.

Watu 3,000 waliuawa kwenye mapigano ya baada ya uchaguzi yaliyopelekea Ouattara kuingia madarakani 2011.

Mapigano hayo yalizuka baada ya Rais Laurent Gbagbo kukataa kukubali ushindi wa Bw Ouattara kwenye uchaguzi huo wa 2010.

Bw Gbagbo alifurushwa madarakani na kukamatwa na sasa anazuiliwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita (ICC).

Mwandishi wa BBC Leone Ouedraogo anasema kuna wasiwasi mjini Abidjan kwamba huenda wapiga kura wengi wasijitokeze kupiga kura.

Watatu kati ya wagombea kumi wa upinzani, akiwemo waziri mkuu wa zamani Charles Konan Banny, wamejiondoa kwenye uchaguzi huo.

Wanadai Ouattara, ambaye alifanya kazi zamani kama mwanauchumi katika Shirika la Fedha Duniani (IMF), ameiba kura kuhakikisha anashinda.

Amekanusha madai hayo na kutoa wito kwa watu kujitokeza kwa wingi.

Wengi bado wanakumbuka yaliyojiti wakati wa vita vilivyotokana na uchaguzi wa mwaka 2010, hasa katika ngome za Bw Gbagbo, waandishi wa habari wanasema.