Diamond Platinumz atuzwa na MTV EMA Milan

Image caption Msanii wa bongo, Nasibu Abdul maarufu ‘Diamond Platnumz

Msanii kutoka bongo, Nasibu Abdul al maarufu '‘Diamond Platinumz'', amewabwaga wasanii wengine wa Afrika na India na kuondoka na tuzo la onyesho bora yaani Best African/Indian Act.

Hii ni kufuatia ushindani mkali uliowavutia wasanii wengine kama vile Yemi Alade, AKA, Davido, DJ Arafat, Indus Creed, Monica Dogra, Priyanka Chopra, The Ska Vengers, Your Chin na Asia.

Diamond alikuwa jukwaani pamoja na wasanii wengine tajika duniani akiwemo Justin Beiber ili kupokea tuzo hiyo kwenye hafla iliyoandaliwa katika uwanja wa Mediolanum Forum mjini Milan, Italia.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Mbali na Diamond, wasanii wengine walioshinda ni Rihanna na Justin Bieber

Mbali na Diamond, wasanii wengine walioshinda ni Rihanna, aliyezawadiwa tuzo la mwanmuziki bora wa kike, Nicki Minaj aliyetawazwa msanii bora wa muziki wa hip hop, huku wimbo wa Bad Blood uliyoimbwa na Taylor Swift akishirikiana Kendrick Lamar ukituzwa kuwa wimbo bora.

Msanii huyo ambaye anajulikana kama baba Tiffah ameongeza idadi ya mataji aliyonyakua chini ya muda wa mwezi mmoja baada ya kuondoka na tuzo tatu kwenye matuzo ya wanamuziki ya Afrimma ambapo alinyakua mataji kadhaa kama vileo video bora ya densi, msanii bora wa Afrika, na msanii bora wa Afrika Mashariki.