Mihadarati:Mwanamfalme wa Saudia akamatwa

Image caption Walinasa mikoba 40 iliyokuwa na tembe hizo zilizopigwa marufuku ilipokuwa ikipakiwa kwenye ndege hiyo ya kibinafsi

Maafisa wa kupambana na matumizi na ulanguzi wa mihadarati nchini Lebanon wamekamata watu watano raia ya wa Saudi Arabia waliokuwa wakijaribu kulangua tani 2 ya mihadarati wakitumia ndege ya kibinafsi inayodhaniwa kuwa mali ya mwanamfalme wa Saudi Arabia.

Kati ya watano hao inadaiwa kuwa mmoja ni mwanamfalme.

Maafisa wa utawala katika uwanja wa ndege wa Beirut walitibua njama ya 5 hao ya kusafirisha mihadarati hiyo walipogundua kuwa mikoba yote iliyokuwa inadhaniwa kuwa na mavazi ilikuwa imejaa tembe zilizopachikwa nembo ya Captagon.

Captagon yenye asili yake nchini Syria inajumuisha viungo vyenye amphetamine na caffeine.

Viungo hivyo vinawafanya watumizi wake wajawe na jazba na hivyo kupendelewa sana na wapiganaji nchini Syria.

Hata hivyo umoja wa mataifa uliiharamishwa kwa sababu inawafanya watumizi wake kuwa mateja.

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Mauzo ya tembe hizo za Captagon Mashariki ya Kati ndiyo inayolaumiwa kwa kufadhili vita vinayoendelea nchini Syria.

Mauzo ya tembe hizo za Captagon Mashariki ya Kati ndiyo inayolaumiwa kwa kufadhili vita vinayoendelea nchini Syria.

Inadhaniwa kuwa watengenezaji wa dawa hiyo haramu wanapata mabilioni ya fedha.

Maafisa wa utawala wanasema kuwa walinasa mikoba 40 iliyokuwa na tembe hizo zilizopigwa marufuku ilipokuwa ikipakiwa kwenye ndege hiyo ya kibinafsi iliyokuwa inaelekea Hael, kaskazini mwa Saudi Arabia.

Hii si mara ya kwanza kwa utawala wa Beirut kunasa shehena kama hiyo ya mihadarati aina ya Captagon.

Mwaka wa 2014 utawala ulinasa takriban tembe milioni 15 za Captagon zilizokuwa zimefichwa na mahindi katika masanduku yaliyokuwa yakisafirishwa kupitia bandari ya Beirut.