Marekebisho ya katiba yaidhinishwa Congo-Brazzaville

Nguesso Haki miliki ya picha
Image caption Sassou Nguesso ameongoza Congo-Brazzaville kwa miaka 30

Wapiga kura katika Jamhuri ya Congo wameidhinisha marekebisho ya katiba yanayomruhusu rais wa sasa kuwania kwa muhula wa tatu.

Kwa mujibu wa matokeo rasmi, asilimia 92 ya wapiga kura walioshiriki kura ya maamuzi kuhusu marekebisho hayo ya kikatiba Jumapili waliunga mkono marekebisho hayo.

Kuandaliwa kwa kura hiyo ya maamuzi kulikuwa kumezua maandamano wiki iliyopita na vyama vikuu vya upinzani viliisusia.

Muungano wa Ulaya na Marekani zimekashifu kuandaliwa kwa kura hiyo, na kusema mazingra nchini Congo hayakuwa mwafaka kuwezesha kuandaliwa kwa kura ya maamuzi huru na ya haki.

Mwandishi wa BBC katika taifa jirani la DR Congo Maud Jullien anasema takwimu kutoka kwa tume ya taifa ya uchaguzi zinaonyesha zaidi ya asilimia 70 ya wapiga kura walishiriki.

Lakini kiongozi wa upinzani ameambia BBC kwamba hawatambui matokeo hayo na kudai kwamba kulikuwa na udanganyifu. Amesema watu wengi hawakujitokeza kupiga kura.

Chini ya katiba ambayo imekuwepo, Rais Denis Sassou Nguesso alikuwa haruhusiwi kuwania kwa muhula mwingine kwa sababu amepitisha umri wa miaka 71 na pia amehudumu mihula miwili tayari.

Image caption Kulikuwa na wengine walioandamana kumuunga mkono

Rais Sassou Nguesso aliingia mamlakani mara ya kwanza mwaka 1979.

Kwa sasa anamalizika muhula wa pili wa miaka saba. Alishinda uchaguzi mkuu wa majuzi zaidi 2009 kwa karibu asilimia 79. Uchaguzi huo ulisusiwa na nusu ya wagombea wa upinzani.

Rais Sassou Nguesso ni miongoni mwa viongozi wa sasa Afrika waliokaa madarakani muda mrefu zaidi.