Askari aliyeburura mweusi afutwa kazi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Fields alituzwa majuzi kwa nidhamu nzuri

Askari polisi mzungu aliyemburura mwanafunzi mweusi huko Marekani alipokaidi amri ya mwalimu ya kumtaka apeane simu yake amefutwa kazi.

Ben Fields, amepigwa chini na jimbo la South Carolina baada ya video kusambazwa katika mitandao ya kijamii ikimuonesha akimburura msichana mweusi mwanafunzi wa shule ya Spring Valley ,Columbia.

Katika video hiyo,Fields anaonekana akimtosa binti huyo sakafuni kwa nguvu na kisha kumbana kama vile wanavyobanwa magaidi wanapokamatwa na polisi.

Yamkini Fields aliitwa na mwalimu ambaye alikuwa akifunza kisha akamfumania mwanafunzi huyo akitumia simu yake darasani kinyume cha sheria.

Mwanafunzi huyo alikaidi amri ya kupeana simu hiyo ama kuondoka darasani.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mwanafunzi mwenzake ndiye aliyechukua video ya tukio hilo

Kauli hiyo ilimgadhabisha mno mwalimu huyo na kusababisha atafute msaada kutoka kwa askari huyo.

Hapo ndipo Fields alitumia nguvu kupita kiasi dhidi ya mwanafunzi huyo wa kike alipokataa kuondoka darasani.

Fields alimweleza kuwa amemkamata.

Alimtosa chini kwa nguvu.

Mwanafunzi mwenzake ndiye aliyechukua video ya tukio hilo kwa simu na kusambaza kwenye mitandao ya kijamii.

Tukio hilo limeibua hisia kali huku wanaharakati wa kupigania haki za watu weusi nchini Marekani wakidai kuwa afisa huyo wa polisi alitumia nguvu kupita kiasi kwa sababu alikuwa ni mwanafunzi mweusi.

Aidha makundi ya wazazi pia wamelalamikia matumizi ya polisi dhidi ya wanafunzi.