Ouattara aahidi maridhiano Ivory Coast

Ouattara Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ouattara amefanikiwa kufufua uchumi wa Ivory Coast

Rais wa Ivory Coast Alassane Ouattara amehutubia taifa hilo kupitia runinga siku moja baada yake kutangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais uliofanywa Jumapili.

Ameahidi kuangazia maridhiano na utekelezaji wa haki.

Ufanisi ni “moja ya viungo vitakavyosaidia katika maridhiano,” alisema, akigusia kujikwamua kwa uchumi wa taifa hilo chini ya uongozi wake.

Lakini alisema haki lazima ipewe nafasi na waathiriwa walipwe fidia, mwandishi wa BBC Tamasin Ford anasema.

Rais huyo amekosolewa na wengi kwa kupendelea upande mmoja katika kutekeleza haki, na kwa kutoangazia maridhiano baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe kuzuka kufuatia uchaguzi mkuu wa 2010.

Akirejelea vyama vya upinzani, amesema ni lazima vitekeleze jukumu lao kama upinzani lakini akafutilia mbali uwezekano wake wa kuunda serikali ya umoja wa kitaifa au serikali ya muungano.

„Serikali za mpito na za umoja wa kitaifa, kwa jumla, huwa hazifanikiwi sana,” alisema.

Mgombea mkuu wa upinzani Pascal Affi N'Guessan wa chama cha FPI, alimpongeza kwa ushindi lakini akasema kura nying alizoshinda nazo ni ishara kwamba hakuna demokrasia halisi humo.