Paul Ryan ateuliwa spika wa bunge Marekani

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Ryan amesema ni heshima kubwa sana kwake kuchaguliwa spika

Mwanasiasa wa chama cha Republican nchini Marekani Paul Ryan ameteuliwa kuwa Spika wa Bunge la Wawakilishi nchini Marekani.

Ryan, anayetoka jimbo la Wisconsin, hakutaka sana kuwania mwanzoni lakini mwishowe alijitosa kwenye kinyang’anyiro na akaungwa mkono na wengi wa wabunge wa Republican katika Bunge la Congress kumrithi John Boehner aliyetoka Ohio.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 45 alikuwa mgombea mwenza wa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha Republican Mitt Romney mwaka 2012.

Amesaidia kuamua sera ya bajeti na uchumi katika bunge la Congress na amesema alitaka kuchukua wadhifa huo ili kuunganisha wanachama wa chama cha Republican.

Haki miliki ya picha AP
Image caption Mitt Romney (kushoto) akiwa na Paul Ryan

Kwenye wadhifa huo wake mpya, yeye ndiye wa pili sasa katika safu ya wanaoweza kumrithi rais nyuma ya makamu wa rais.

Miongoni mwa majukumu mengine, spika wa bunge nchini Marekani husimamia shughuli za bunge la chini la Congress katika masuala ya kiutawala na kibiashara.