Jengo labomoka na kuua watu 17 Uchina

Haki miliki ya picha xinhua
Image caption Msingi wa jengo hilo ulikuwa unafanyiwa ukarabati

Jengo la ghorofa mbili limebomoka katika mkoa wa Henan, katikati mwa Uchina na kuua wafanyakazi mjengo 17 na kujeruhi wengine 23, vyombo vya habari vya serikali vimeripoti.

Maafisa wa uokoaji wamekuwa wakifanya kazi usiku kucha kuondoa miili ya waliofariki pamoja na kutoa majeruhi kutoka kwenye vifusi.

Mkasa huo umetokea katika eneo la Beiwudu, wilaya ya Wuyang.

Tisa kati ya waliojeruhiwa wanatibiwa katika hospitali iliyoko mji wa Luohe, na wamo katika hali mahututi, maafisa wamesema.

Maafisa hao wamesema wafanyakazi hao wa mjengo walikuwa wakifanyia ukarabati msingi wa jumba hilo ajali hiyo ilipotokea.

Serikali ya wilaya ya Wuyang sasa imesitisha juhudi za uokoaji.

Uchunguzi umeanza kuhusu nini hasa kilichosababisha mkasa huo ambao umeibua tena wasiwasi kuhusu kutekelezwa kwa kanuni za usalama kuhusu majengo nchini Uchina.

Haki miliki ya picha Reuters

Mwezi Mei, jumba la kutunza wazee liliteketea mkoani Henan na kuua watu 38. Ilibainika baadaye kwamba jumba hilo lilijengwa vibaya kwa kutumia vitu vinavyoshika moto haraka.

Mmoja wa manusura aliambia kituo cha runinga cha serikali cha CCTV kwamba wafanyakazi hao walitoka mji wa Nanyang kusini-magharibi mwa mkoa wa Henan.

Jengo hilo lilijengwa miaka ya 1990.