Urusi yaonya kuhusu hatari ya vita Syria

Lavrov Haki miliki ya picha AFP
Image caption Lavrov alizungumza baada ya kukutana na Kerry

Urusi imeonya kuwa kuna hatari ya kuzuka kwa “vita vya mawakala” eneo la Mashariki ya Kati baada ya Marekani kusema itawatuma wanajeshi maalum kusaidia waasi Syria.

Vita vya mawakala ni vita ambavyo huhusisha makundi yanayoungwa mkono na mataifa makubwa kupigana, bila mataifa hayo kupigana moja kwa moja.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Urusi Sergei Lavrov alisema hilo linazidisha haja ya Marekani kufanya kazi kwa pamoja na Urusi.

Maafisa wa Marekani wamesema “wanajeshi chini ya 50” watatoa mafunzo, kushauri na kusaidia vikosi vya makundi yanayopigana dhidi ya Islamic State (IS).

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa wanajeshi wa Marekani kuhudumu ardhini nchini Syria.

Bw Lavrov amesema Marekani ilifanya uamuzi huo bila kushauriana na viongozi wa Syria.

“Nina uhakika Marekani na Urusi hazitaki vita hivi vigeuke na kuwa vita vya matarishi. Lakini kwangu ni wazi kwamba hili linazidisha umuhimu wa kuwa na ushirikiano wa kijeshi.”

Alikuwa akizungumza baada ya kushauriana na Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani John Kerry na balozi wa UN nchini Syria Staffan de Mistura mjini Vienna.

"Lengo letu kuu ni kuwezesha vikosi vinavyopigana Syria lakini je, hilo linawaweka wanajeshi wa Marekani hatarini? Naam, hakuna shaka kuhusu hilo,” Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ash Carter aliambia wanahabari baadaye.

Hakufutilia mbali uwezekano wa kupeleka wanajeshi zaidi iwapo mpango huu wa sasa utafanikiwa.

Majuzi, Marekani ilitupilia mbali mpango wake wa kutoa mafunzo kwa waasi nchini Syria, na badala yake kuanza kuwapa viongozi wa waasi silaha na vifaa moja kwa moja.

Msemaji wa ikulu ya White House Josh Earnest amesema Rais Obama anataka kutoa usaidizi zaidi kwa wapiganaji waasi ambao wanafanikiwa vitani.