Miili ya waliofariki ajalini Sinai yapelekwa Urusi

Haki miliki ya picha epa
Image caption Mabaki ya ndege ya Urusi iliyoangukwa Misri

Miili ya watu 160 waliofariki dunia katika ajali ya ndege eneo la Sinai nchini Misri imewasili mjini St Petersburg nchini Urusi

Katika ajali hiyo ya ndege iliyotokea siku ya Jumamosi eneo la Sinai watu wote 224 waliokuwa katika ndege hiyo walikufa.

Rais wa Misri Abdel Fattah al Sisi amewataka watu wote wawe na uvumilivu wakati uchunguzi ukiendelea.

Mmoja wa wachunguzi wa masuala ya safari za ndege kutoka Urusi amesema kuwa ndege ya Urusi iliyoanguka katika rasi ya Sinai nchini Misri ilivunjika ikiwa hewani.

Aleksandr Neradko amesema kwamba mabaki ya ndege hiyo yametapakaa katika rasi ya Sinai.

Wengi wa abiria waliokuwa kwenye ndege hiyo ni raia wa Urusi.

Mchunguzi kutoka nchini Urusi amesema kwamba ni mapema mno kujua chanzo cha ajali hiyo.

Wapiganaji wa kundi la Kiislamu la Islamic State walikuwa wamedai kudungua ndege hiyo, madai ambayo yamepingwa na serikali za Urusi na Misri.

Nchini Urusi kulikuwa na siku ya maombolezo ya kitaifa Jumapili.