Majaji waidhinisha ushindi wa Ouattara Ivory Coast

Ouattara Haki miliki ya picha
Image caption Ouattara amesifiwa kwa kufufua uchumi wa taifa hilo

Majaji wa mahakama ya kikatiba nchini Ivory Coast wamethibitisha Rais Alassane Ouattara ndiye mshindi wa uchaguzi mkuu uliofanyika siku nane zilizopita.

Kiongozi huyo alipata ushindi mkubwa kwenye uchaguzi huo.

"Ni haki kumtangaza kuwa rais aliyechaguliwa,” jaji mkuu wa mahakama hiyo Mamadou Kone amesema, kama alivyonukuliwa na shirika la habari la AFP.

Bw Ouattara alichaguliwa kuongoza kwa muhula wa pili baada ya kupata 84% ya kura ikilinganishwa na 9% alizopata mpinzani wake mkuu Pascal Affi N'Guessan.

Image caption Uchaguzi mkuu Ivory Coast ulifanyika Oktoba 25

Baadhi ya viongozi wa upinzani walisusia uchaguzi huo, wakidai kulikuwa na udanganyifu.

Bw Ouattara alichukua uongozi baada ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyosababisha vifo vya watu 3,000 baada ya uchaguzi mkuu 2010.

Mtangulizi wake, Laurent Gbagbo, aliyekataa kushinda baada ya uchaguzi huo, anazuiliwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, ambako amefunguliwa mashtaka ya kuchochea vita hivyo.

Anakanusha mashtaka hayo.