Kesi dhidi ya Pistorius yasikizwa upya

Haki miliki ya picha AP
Image caption Oscar Pistous

Mahakama kuu ya rufaa nchini Afrika Kusini imekamilisha kusikiza tena kesi inayomhusu mwanariadha mlemavu, Oscar Pistorius ambaye anatuhumiwa kumuuwa mpenziwe wa kike Reeva Steenkamp.

Mahakama hiyo ilikuwa iamue iwapo Pistorius aliiuwa makusudi au bila kukusudia, wakati alipomfyatulia risasi mpenziwe wakati sikukuu ya wapendanao mnamo mwaka 2013.

Muendesha mashtaka Gerrie Nel, ameiambia mahakama kuwa kesi ya awali ilishindwa kuchunguza kwa makini ushahidi wote uliotolewa.

Oscar Pistorius aliachiliwa huru mwezi uliopita na kupata kifungo cha nyumbani.

Wakati huo alikuwa ametumikia kifungo cha mwaka mmoja tu gerezani kati ya tano alizohukumiwa kwa kumuua Reeva Steenkamp.

Endapo mahakama hiyo kuu ya rufaa itabatilisha uamuzi wa awali na kumshtaki kwa kesi ya mauaji, mwanariadha huyo bingwa wa mbio za matimko huenda akarejeshwa tena jela na kutumikia kifungo cha miaka kumi na mitano.

Hakuna tarehe kamili iliyotolewa kwa uamuzi.

Ni takribani siku arobaini tangu mwanariadha huyo alipooachiwa kutoka jela kutumikia kifungo cha nyumbani.

Oscar Pistorius ana uwezekano kukabiliwa na kifungo cha muda mrefu.

Haki miliki ya picha BBC World Service
Image caption Marehemu Reeva Steenkamp

Kama upande wa mashtaka ambayo ni Jamhuri itashinda kwenye rufaa kosa la mwanariadha huyo litabadilika na kutoka kosa la kuua bila kukusudia na kuwa kosa la mauaji.

Pistorius mwenye umri wa miaka 28 hakuwepo mahakamani.

Anafuatilia kesi yake kutoka katika nyumba ya kifahari ya mjomba wake iliyopo Pretoria ambapo anamalizia kifungo cha miaka minne kilichobaki.

Hajajulikana nini kitakachotokea katika kesi hiyo inayosikilizwa na majaji watano lakini ifahamike masuala ya kisheria ni ya kiufundi zaidi.

Hoja za Upande wa mashataka ambayo ni Jamuhuri ni kwamba Jaji aliyesikiliza kesi hiyo Thokozile Masipa hakuwa sahihi kuona kuwa mwanariadha huyo alitenda kosa la mauaji ya kutokusudia kwa madai kwamba mwanaridha alijua madhara ya tendo alilolifanya.

Pistorius anatuhumiwa kufyatua risasi mara nne kwenye bafu iliyokuwa imefungwa na alijua tendo hilo lingeweza kusababisha kifo.

Hata hivyo mwanariadha huyo amekuwa akijitetea kuwa alidhani kuwa alikuwa amevamiwa na wezi na kwamba alidhani mpenzi wake Reeva Steenkamp alikuwa yupo chumbani.

Upande wa mashataka unapinga kuwa hoja na kusema mwanariadha huyo alikusudia kuua.