Al Qaeda wapigwa na kimbunga Yemen

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Al Qaeda wapigwa na kimbunga Yemen

Kimbunga cha aina yake kimepiga maeneo yanayothibitiwa na wanamgambo wa Al-Qaeda katika pwani ya bahari ya Arabia huko Yemen.

Maelfu wamekimbia mji wa Mukalla, mahala ambapo maji yalizamisha magari yaliyokuwa yameegeshwa barabarani.

Kimbunga hicho kiitwacho Chapala kimebomoa majengo yaliyoko mkabala na bahari.

Upepo mkali unaokwenda kwa kasi ya kilomita 100 kwa saa, umeiacha mji huo wa tano kwa ukubwa nchini Yemen bila ya umeme.

Taarifa za kutokea maafa bado hazijatolewa kufikia sasa.

Kimbunga hicho na upepo huo ndio mkali zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Yemen kwa miongo kadhaa.

Shughuli za kusambaza msaada wa chakula zitatatizwa na umasikini uliokithiri pamoja na vita vya wenyewe kwa wenyewe.