Aliyetoweka baada ya kumaliza mbio apatikana

Marengo Haki miliki ya picha AP
Image caption Marengo alipatikana akiwa bado amevalia mavazi ya mbio

Mwanariadha kutoka Italia aliyetoweka baada ya kumaliza mbio za New York Marathon amepatikana.

Gianclaudio Marengo, anayejaribu kujinasua kutoka kwa uraibu wa kutumia dawa za kulevya aina ya heroini, alipatikana naafisa wa polisi ambaye hakuwa kazini akiwa bado amevalia mavazi ya kushiriki mbio.

Marengo, 30, alionekana mara ya mwisho karibu na Central Park Jumapili muda mfupi baada yake kumaliza mbio hizo kwa kutumia muda was aa nne na dakika 44.

Marengo, ambaye haelewi Kiingereza, alikuwa akikimbia kwa niaba ya kituo cha kurekebisha tabia waraibu wa dawa Italia cha San Patrignano.

Kituo hicho kilisema Marengo alikuwa kwenye kundi la waraibu wanane lakini walitengana kwa sababu kila mmoja alitumia muda tofauti kumaliza mbio hizo.

“Ni mtu dhaifu sana na anayetekwa na hisia ambaye baada ya kuwa mraibu wa dawa kwa miaka mingi alipata nafasi ya kurekebisha katika San Patrignano," kituo hicho kilisema kupitia taarifa.

Wakenya Stanley Biwott na Mary Keitany walishinda mbio hizo upande wa wanaume na wanawake mtawalia.