Ndege yaanguka Sudan Kusini

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ndege hiyo ilianguka muda mfupi baada ya kupaa

Ndege ya kubeba mizigo ilianguka muda mfupi baada ya kupaa kutoka uwanja wa ndege wa Juba, Sudan Kusini na kuua watu zaidi ya 25.

Kuna wasiwasi huenda idadi hiyo ikaongezeka.

Msemaji wa rais wa Sudan Kusini Ateny Wek Ateny ameambia shirika la habari la Reuters kwamba mhudumu mmoja wa ndege hiyo pamoja na mtoto, ambao walikuwa kwenye ndege hiyo, wamenusurika.

Ndege hiyo aina ya Antonov An-12, iliyokuwa safarini kuelekea mji wa Paloch katika jimbo la Upper Nile ilipoanguka mika 800 kutoka uwanja huo wa ndege katika ukingo wa mashariki wa Mto Nile.

Kulikuwa na habari za kutatanisha kuhusu idadi ya waliofariki, shirika la habari la Reuters likinukuu afisa mmoja wa polisi na mtu aliyeshuhudia ajali hiyo wote wawili wakisema waliona miili 41 eneo la ajali.

Shirika la habari la AFP lilimnukuu afisa wa Shirika la Msalaba Mwekundu aliyesema miili ya watu 36 imechukuliwa na kupelekwa chumba cha kuhifadhia maiti.

Bw Ateny alisema ndege hiyo ilikuwa imebeba watu 18, wakiwemo wahudumu sita wa ndege.

Alisema abiria wote walitoka Sudan Kusini.

Alidokeza kwamba huenda idadi ya waliofariki ikaongezeka kwani kunao waliofariki ardhini baada ya kuangukiwa na ndege hiyo.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Ndege za kubeba mizigo wakati mwingine pia hubeba abiria Sudan Kusini

Bw Ateny alisema wahudumu watano wa ndege hiyo walikuwa kutoka Armenia na mmoja kutoka Urusi. Wizara ya mashauri ya kigeni ya Armenia imethibitisha kuwa raia wake watano walifariki.

Ndege hiyo ilifanya ziara ya kwanza 1971 na ilikuwa inamilikiwa na kampuni ya Asia Airways kutoka Tajikistan, wizara ya uchukuzi ya Tajikistan iliambia shirika la habari la Ozodagon. Hata hivyo ilikuwa ikitumiwa na kampuni ya Allied Services inayohudumu nchini Sudan Kusini.

Ajali hiyo imetokea siku chache tu baada ya ndege nyingine ya Urusi kuanguka eneo la Sinai, Misri Jumamosi.