Runinga yatafuta msichana wa kuigiza Nicki Minaj

Nicki Minaj Haki miliki ya picha Getty
Image caption Nicki Minaj alizaliwa Trinidad

Kituo cha runinga cha ABC Family kimetangaza kwamba kitaandaa mahojiano mtandaoni kumtafuta msichana atakayemuigiza Nicki Minaj.

Msichana atakayefanikiwa, atamuigiza Minaj alipokuwa mdogo kwenye filamu ya ucheshi ya nusu saa kuhusu maisha ya mwanamuziki huyo wa kufoka.

Filamu hiyo itaangazia maisha ya Minaj alipokuwa msichana mdogo mtaa wa Queens, New York miaka ya 1990 baada ya familia hiyo kuhamia mtaa huo kutoka Trinidad.

Msichana anayetafutwa anafaa kuwa na umri wa kati ya miaka 11 na 13

Nicki Minaj ndiye atakayesimamia filamu hiyo na pia ataandika mistari ya kutumiwa na msichana atakayemuigiza kwenye nyimbo za kufoka, yaani rap.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Nicki Minaj ndiye atakayesimamia utengenezaji wa filamu hiyo

Maelezo kuhusu jinsi ya kuwasilisha maombi na kushiriki yamewekwa kwenye app ya Disney Applause na siku ya mwisho ni Novemba 15.

Nicki Minaj, ambaye jina lake halisi ni Onika Tanya Maraj, ana umri wa miaka 32 na anafahamika sana kwa nyimbo kama vile Anaconda, Bang Bang na Truffle Butter. Amependekezwa kuwania tuzo za Grammy mara saba.

Kituo cha ABC Family kimepanga kubadilisha jina na kuanza kuitwa Freeform Januari mwakani.