Siku ya kuapishwa kwa Magufuli kuwa sikukuu

Magufuli KIkwete
Image caption Rais Kikwete anaondoka madarakani baada ya kuongoza mihula miwili

Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ametangaza siku ya kuapishwa kwa rais mpya hapo kesho kuwa sikukuu.

Kupitia taarifa, Rais Kikwete amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha Watanzania kushiriki katika sherehe ya kumwapisha kiongozi mpya.

“Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt Jakaya Mrisho Kikwete ameamua na ameitangaza kesho, Alhamisi, Novemba 5, mwaka huu, 2015, kuwa Sikukuu na siku ya mapumziko” imesema taarifa kutoka ikulu.

“Rais Kikwete amefanya uamuzi huo, ili kuwawezesha Watanzania kushiriki katika sherehe za kuhitimisha Uongozi wa Serikali ya Awamu ya Nne na kuingizwa madarakani Mheshimiwa Dkt John Pombe Joseph Magufuli kuwa Rais wa Tano wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”

Rais Kikwete, kupitia taarifa iliyotolewa na Ofisi ya Katibu Mkuu Kiongozi (KMK) kupitia Bw Ombeni Yohana Sefue, amesema amechukua hatua hiyo “kwa mujibu wa mamlaka aliyo nayo chini ya Kifungu cha 3 cha Sheria ya Sikukuu za Kitaifa.”

Bw Magufuli alitangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania kuwa mshindi wa uchaguzi wa urais Alhamisi wiki jana, uamuzi iliyopingwa na chama cha upinzani Chadema.