Zuma kuhudhuria sherehe ya kumuapisha Magufuli

Zuma Haki miliki ya picha AP
Image caption Zuma ataandamana na waziri wa ushirikiano wa kimataifa Afrika Kusini

Kiongozi wa Afrika Kusini Jacob Zuma ni miongoni mwa viongozi wa mataifa mbalimbali duniani watakaohudhuria sherehe ya kuapishwa kwa rais mpya Tanzania.

Kwa mujibu wa taaifa kutoka afisi yake, Rais Zuma ataandamana na Bi Maite Nkoana-Mashabane, ambaye ni waziri wa uhusiano na ushirikiano wa kimataifa Afrika Kusini.

Mgombea wa CCM John Pombe Magufuli alitangazwa mshindi wa uchaguzi wa urais nchini Tanzania Alhamisi wiki iliyopita.

Kwa mujibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania, Bw Magufuli alipata asilimia 58 ya kura zilizopigwa kwenye uchaguzi huo uliofanyika Oktoba 25.

Mgombea urais kutoka chama cha Chadema Edward Lowassa alipinga matokeo hayo akisema lipokonywa ushindi.

Mhubiri mashuhuri kutoka Nigeria TB Joshua, ni mmoja wa wageni ambao tayari wamewasili Tanzania kwa sherehe hiyo.

Waziri mkuu wa zamani wa Kenya, Bw Raila Odinga, ambaye kwa sasa ndiye kiongozi mkuu wa upinzani pia yumo Tanzania.

Bw Odinga, ambaye ni rafiki wa karibu wa Bw Magufuli, leo alikutana na rais wa zamani wa Tanzania Benjamin Mukapa, aliyemtangulia Rais anayeondoka mamlakani Jakaya Kikwete.