Changamoto sita kuu zinazomsubiri Magufuli

Magufuli
Image caption Magufuli anakabiliwa na changamoto kadha

Rais mteule wa Tanzania John Pombe Magufuli ameapishwa leo baada ya ushindi wake katika uchaguzi uliotajwa kuwa wenye ushindani zaidi katika historia ya Tanzania.

Akijulikana kama ‘Tingatinga’, Magufuli alishinda kwa kupata asilimia 58.46 ya kura huku hasimu wake mkubwa Edward Lowassa akipata asilimia 39.97 ya kura.

Ushindi wa Magufuli ulipokelewa kwa hisia tofauti, kwani hata kama kura nyingi za maoni zilionyesha kuwa angeshinda, wachambuzi wengi wa masuala ya kisiasa walikuwa na wakati mgumu kubashiri nani hasa atashinda hasa wakizingatia namna ushindani ulivyokuwa mkali baada ya vyama vinne vya upinzani kuungana na kumsimamisha Lowassa kama mgombea wao wa Urais.

Kwa kiasi kikubwa, Magufuli alibebwa na umaarufu wake binafsi zaidi ya ule wa chama chake Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambacho kimekuwepo madarakani tangu uhuru wa Tanzania mnamo mwaka 1961, ingawa kilipata jina la sasa 1977 baada ya kuungana kwa Tanu na chama cha Afro Shirazi cha Zanzibar.

Uchaguzi umekwisha sasa, kazi imebaki kwa mtu mmoja, Magufuli. Ama kwa hakika yapo mambo lukuki yanayohitaji uongozi wake uyashughulikie, lakini yafuatayo ni baadhi ya mambo ambayo ushughulikiaji wake ndio utakaopelekea namna uongozi wake utakumbukwa hapo baadaye, kama anavyochanganua mwandishi wa BBC Sammy Awami.

1. Rushwa

Image caption Magufuli ameahidi kuunda mahakama maalum ya kushughulikia mafisadi

‘Mabadiliko’ ni neno lililotawala kila kona wakati wa pilika pilika za kampeni, katika kambi za upinzani na hata chama tawala.

Na sasa kwa kuwa Magufuli ndio amepewa jukumu kuongoza nchi, Watanzania wanategemea kazi ya kwanza atakayoifanya ni ‘kusafisha nyumba’.

Akiwa kama ‘mkuu wa kaya’, Magufuli anatarajiwa kuweka kipaumbele katika kuwashughulikia wala rushwa na mianya ya rusha yenyewe.

Bila shaka hii haitakuwa kazi rahisi. Wapo viongozi wengi wa umma na wale wa chama chake ambao kuwa kwao madarakani kwa muda mrefu kumewawezesha kujijengea mazingira ya kujinufaisha bila kuwa na wasiwasi wa kugundulika na kuadhibiwa.

Lakini tangu siku ya uzinduzi wa kampeni, Magufuli mwenyewe aliahidi kwamba ataanzisha mahakama maalum ya rushwa ili mafisadi wadhibitiwe ipasavyo na kwa kasi itakayoridhisha. Na kwa kiasi kikubwa kuchaguliwa kwake kumetokana na imani ya Watanzania wengi kwamba anayo nia ya kupambana na hali ya rushwa iliyokithiri

Kipimo cha kwanza kabisa kitakuwa katika uundwaji wa baraza lake la mawaziri. Je, litahusisha watu ambao hawana madoa ya rushwa? Watakuwa ni watu wenye sifa ya uchapakazi? Bila shaka haya ndio maswali yanayogonga vichwa vya wananchi wengi hivi sasa.

Kwa hakika utakuwa ni mtihani wake mgumu wa kisiasa, lakini wengi wa waliompigia kura wanaamini kwamba anauthubutu wa kufanya maamuzi magumu

2. Vijana na Ajira

Image caption Vijana wengi wanataka ajira

Vijana wamefanyika chachu kubwa sana katika uchaguzi huu ulioisha. Wengi wao waliamini kwamba kura yao ni ya muhimu na ina uwezo mkubwa wa kuleta mabadiliko. Na si vigumu sana kujua kwa nini vijana hawa walihamasika kiasi hicho.

Takribani nusu ya Watanzania zaidi ya milioni 50 ni vijana, na hili ndio kundi linaloathirika zaidi na ukosefu wa ajira nchini

Takwimu rasmi za serikali zinasema ukosefu wa ajira upo kwa asilimia 10, lakini mara nyingi watu hudhani tatizo ni kubwa zaidi ya hapo.

Wengine watakumbuka lile tangazo la kazi la siku chache zilizopita katika idara ya uhamiaji. Kwa nafasi 70 za kazi, maombi yaliyopatikana yalikuwa 10,000. Hata udahili ilibidi ufanyike katika uwanja wa taifa wa mpira.

Magufuli anabeba mzigo mkubwa wa kuhakikisha vijana hawa wengi waliojitokeza kupiga kura wanafunguliwa milango ya kupata nafasi za ajira. Labda kupitia ahadi yake ya kufufua na kuanzisha viwanda vipya inaweza kutatua uhitaji huu

3. Elimu

Image caption Suala la elimu lilitawala mikutano ya kampeni

Wakati upinzani ukiahidi elimu ya bure kuanzia chekechea hadi chuo kikuu, Magufuli yeye aliahidi elimu bure kuanzia chekechea hadi sekondari, kidato cha nne tu.

Elimu ni moja ya ahadi ambazo ziliwekewa mkazo na pande zote mbili za ushindani hali inayoonesha uhitaji mkubwa uliopo katika sekta hii.

Wakati Watanzania wengi wakifurahishwa na ahadi ya elimu bure, wengi wao pia hawaridhishwi na ahadi hiyo kuishia hapo tu.

Walimu na maslahi yao, kiwango cha elimu kisichoridhisha, mitaala isiyozalisha wahitimu wenye ujuzi wa kutosha kwa nguvu kazi ya taifa lakini hata ushindani wa nje ya nchi.

Shule nyingi za umma hazina walimu wa kutosha na upungufu mkubwa wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Magufuli anakabiliwa na changamoto ya kuyatatua haya na mengine kadhaa kuhusiana na sekta ya elimu.

4. Katiba Mpya

Image caption Mchakato wa kutafuta Katiba Mpya uliahirishwa hadi baada ya uchaguzi

Rais anayeondoka madarakani Jakaya Kikwete aliahidi katiba mpya, lakini hadi anaondoka madarakani bado haijapatikana huku uratibu wake ukiwa umekwama njiani.

Vyama vya upinzani vilipata uungwaji mkono mkubwa sana vilipoamua kulivalia njuga suala la upatikanaji wa katiba mpya. Lakini wakati wa kampeni zake, Magufuli hakuligusia kabisa suala hili. Swali ni kwamba atakaa kimya hivi kwa muda wake wote wa urais? Si rahisi.

5. Migogoro Visiwani Zanzibar

Image caption Matokeo ya uchaguzi Zanzibar yalifutiliwa mbali na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi visiwani

Mgogoro wa kisiasa unaoendelea visiwani Zanzibar ni kumbukumbu tosha kwamba visiwa hivyo vinauhitaji mkubwa wa mwarobaini utakaokomesha kabisa mizizi ya chokochoko zote zisizoisha kuibuka

Marais wote wanne waliomtangulia Magufuli wameshughulika kwa namna yao kutatua mizozo ya kisiasa visiwani Zanzibar, na wote hawajafanikiwa kukomesha moja kwa moja.

Hakuna muujiza wowote unaotarajiwa kufanywa na Magufuli, lakini hata hivyo hatarajiwi kuukwepa mgogoro wa Zanzibar kwa namna yoyote ile. Kinachosubiriwa tu ni kwamba yeye atatumia njia gani kuushughulikia

6. Chama cha CCM

Image caption Makada wengi wa CCM walihama chama hicho

Yote tisa, kumi ni chama chake alichokitumia kuingia madarakani. Ni wazi kwamba uteuzi wake kupeperusha bendera ya chama hakuungwa mkono asilimia mia moja na wajumbe na wanachama wote wa CCM. Wapo kadhaa ambao walitamani na kuamini kwamba Lowassa ndiye alikuwa anafaa zaidi kuwa mgombea.

Hali hiyo ilisababisha mgongano mkubwa ndani ya chama hicho, na hata kutishia kupasuka kwake. Lakini wakati kimenusurika msambaratiko, chama hicho hakikuweza kukwepa kutoroka kwa makada wake wakubwa kama Lowassa mwenyewe, mwanachama na kiongozi mkongwe Mzee Kingunge Ngombale Mwilu na aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani Fredrick Sumaye pamoja na wabunge wengine kadha.

Bila shaka mtikisiko huu haujaondoka kabisa, na mara tu atakapokabidhiwa kuwa kiongozi wa chama chake, basi atakuwa na kazi ya kuganga majeraha yaliyopo lakini zaidi sana ni kuurejesha umoja na mshikamano wa chama.