UN: Mahasimu Sudan Kusini wanahodhi silaha

Haki miliki ya picha AP
Image caption Serikali na waasi Sudan Kusini watuhumiwa kwa kuendelea kuhodhi silaha na kukiuka mkataba wa amani uliotiwa saini mwezi Agosti.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa imeshutumu serikali na waasi nchini Sudan Kusini kwa kuhodhi silaha na kukiuka mkataba wa amani uliotiwa saini mwezi Agosti.

Ripoti hiyo iliyotolewa na jopo la wataalamu linasema pia kuwa mauaji, ubakaji na uporaji mkubwa unaendelea licha ya pande zote mbili kukubaliana kumaliza takriban miaka miwili ya mapigano ya wenyewe nchini humo.

Jopo hilo la wataalamu lilitoa ripoti yake kwa baraza la usalama la umoja wa mataifa na kusema kuwa pande zote mbili zimekuwa zikinunua silaha licha ya kutia saini mkataba wa amani.

Ripoti hiyo pia inaorodhesha takriban matukio 50 ya ubakaji katika mwezi wa Oktoba pekee.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Pande zote mbili zimekuwa zikinunua silaha

Aidha inasema kumekuwa na uporaji wa mali, uharibifu mkubwa wa mali kwa mfano kuchomwa kwa nyumba na visa vingi vya wizi wa mifugo.

Wataalamu hao wanasema mapigano yameendelea katika sehemu kadhaa nchini Sudan Kusini huku maelfu ya watu wakifurushwa makwao.

Baraza la uslama la umoja wa mataifa limegawanyika kuhusu pendekezo la kuiwekea Sudan Kusini vikwazo huku Urusi ikiyaongoza mataifa mengine ya Afrika kupinga hatua hiyo.

Wakati huohuo, mashirika ya misaada yanasema takriban watu milioni nne sasa wanakabiliwa na tishio kubwa la kiangazi na baa la njaa huku hali ikiendelea kuzorota nchini humo.