Wakenya 20 waagizwa kuondoka Somalia

Wakenya Somalia
Image caption Wakenya hao walikuwa wamekaa Somalia kwa takriban miezi mitano

Mahakama nchini Somalia imewapata Wakenya 22 na hatia ya kuwa nchini humo kinyume cha sheria.

Mwandishi wa BBC aliyeko Mogadishu Ibrahim Aden anasema jaji amewapiga Wakenya hao faini ya $10 (£6.5) kwa kila siku waliyokaa Somalia na wakishindwa kulipa watafungwa jela.

Kampuni iliyowaajiri kazi Wakenya hao katika uwanja wa ndege mjini Mogadishu, kwa jina Labour Link nayo imetozwa faini ya $10,000 (£6,500).

Wakenya wengine watano, ambao hawakuwa kortini pia wametakiwa kulipa faini hiyo.

Wakili wa Wakenya hao Abdiwahid Osman Haji amesema atakata rufaa uamuzi huo wa mahakama.

Hii ni mara ya kwanza katika karibu miongo miwili kwa serikali nchini Somalia kuwachukulia hatua wahamiaji haramu, hasa kutoka taifa jirani la Kenya.

Wengi huenda huko kama wafanyakazi au wafanyabiashara, wakilenga kufaidi kutokana na fursa nyingi zinazopatikana Mogadishu.

Miaka ya hivi karibuni, Kenya imewafurusha raia wengi wa Somalia ikisema ni tishio kwa usalama wake.