Magufuli abadilisha usimamizi wa hospitali kuu

Magufuli Haki miliki ya picha Statehouse Tanzania
Image caption Magufuli amekerwa na utoaji wa huduma hospitali ya Muhimbili, ikulu imesema

Rais wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli leo amefanya ziara nyingine ya kushtukiza, wakati huu katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na kufanyia mabadiliko usimamizi wa hospitali hiyo.

Kiongozi huyo mpya amesikitishwa na kuhuzunishwa na hali ya huduma kwa wagonjwa hususan wanaolala chini, kwa mujibu wa taarifa kutoka ikulu.

“Pia amekasirishwa na hali ya kutokujali wala kushughulikia vifaa vya kufanyia kazi ambapo amekuta mashine muhimu za uchunguzi wa magonjwa kama vile MRI na CT-SCAN zikiwa hazifanyi kazi kwa muda wa miezi miwili sasa, ilihali mashine kama hizo katika Hospitali za binafsi zinafanya kazi na wagonjwa wanaelekezwa kwenda kutafuta huduma huko,” katibu wake mkuu Ombeni Sefue amesema.

Dkt Magufuli ameagiza Hussein Kidanto ambaye amekuwa kaimu mkurugenzi mkuu wa hospitali hiyo aondoke na kurudi Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii ambako atapangiwa kazi nyingine.

Amemteua Prof Lawrence Mseru kuwa mkurugenzi mkuu mpya na kumtaka aripoti kazini kesho.

Rais huyo pia amevunja bodi simamizi ya hospitali hiyo, ambayo ilikuwa tayari imemaliza muda wake wa kuhudumu.

“Rais ametoa wiki moja na kwa vyovyote si zaidi ya wiki mbili kwa uongozi mpya wa Muhimbili kuhakikisha kuwa mashine zote za uchunguzi wa magonjwa ambazo hazifanyi kazi zinafanya kazi na kuhudumia wananchi kama ipasavyo,” anasema Bw Sefue.

Dkt Magufuli aidha ameagiza kuanzia sasa hospitali zote nchini humo ziwe zikitenga fedha kutoka kwenye mapato yao wenyewe na kuhakikisha mashine na vifaa vyote vya kazi vinafanya kazi wakati wote.

Ijumaa wiki iliyopita, siku moja tu baada ya kuapishwa, Dkt Magufuli alifanya ziara ya kushtukiza katika Hazina Kuu ambako alieleza kushangwa kwake na hali kwamba maafisa walikuwa hawamo afisini wakati ambao walifaa kuwahudumia wananchi.