Obama kukutana na Netanyahu Marekani

Obama
Image caption Netanyahu hakufurahishwa na kuafikiwa kwa mkataba wa nyuklia na Iran

Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu watakutana leo kwa mara ya kwanza tangu uhusiano baina yao kudorora kufuatia mwafaka kati ya mataifa yenye ushawishi duniani na Iran kuhusu nyuklia.

Mashauriano hayo mjini Washington yanajiri baada ya wiki za vurugu na makabiliano kati ya Waisraeli na Wapalestina.

Waisraeli sita waliuawa kwa kudungwa visu na Wapalestina Jumapili. Mpalestina aliyechomoa kisu akionekana kulenga kushambulia walinzi wa Israel naye alipigwa risasi na kuuawa Jumatatu.

Bw Netanyahu yumo Marekani kutafuta kuongezwa kwa usaidizi wa kijeshi wa kila mwaka wa Marekani kwa Israel.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kupelekea kuongezwa kwa msaada wa kijeshi kutoka $3.1bn (£2bn) kila mwaka hadi $5bn, ripoti katika vyombo vya habari zinasema.

Uhusiano kati ya Bw Netanyahu na Bw Obama ulidorora Julai baada ya kutiwa saini kwa mkataba wa nyuklia kati ya Marekani nan chi nyingine za Magharibi na Iran ambao ulitiwa saini mwezi Julai. Mwafaka huo ulipingwa vikali na Israel.

Wiki iliyopita, Marekani pia ilieleza kushangazwa kwake na hatua ya Netanyahu kumteua Ran Baratz kuwa msemaji wake. Bw Baratz alikuwa ametoa matamshi ya kukosoa utawala wa Marekani.

Akiandika kwenye Facebook, Bw Baratz alimtuhumu Bw Obama kwa kuwa na chuki dhidi ya Wayahudi na kusema Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Marekani John Kerry ana uwezo wa kufikiria wa mtoto wa chini ya miaka 12.

Msemaji wa wizara ya masuara ya ndani wa Marekani alisema jumbe hizo zilikuwa za kuudhi.

Bw Baratz hakuandamana na Netanyahu kwenye ziara hiyo.