Utata wazidi kuhusu mawaziri Zanzibar

Khamis
Image caption Bw Khamis amesema kikatiba hakuna mawaziri Zanzibar

Utata umezingira hatima ya mawaziri katika serikali ya visiwani Zanzibar baada ya kuongezewa muda kwa rais wa visiwani kutokana na utata kuhusu matokeo ya uchaguzi.

Chama cha Wananchi (CUF) kimepinga hatua ya kumuongezea muda wa kuhudumu Rais Ali Mohamed Shein anayetoka Chama cha Mapinduzi (CCM) wakisema hatua hiyo haikufuata katiba.

Bw Shein aliongezewa muda baada ya mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) Jecha Salim Jecha kufutilia mbali matokeo ya uchaguzi visiwani humo akisema ulijaa udanganyifu.

Lakini chama cha CUF kinasema uchaguzi huo ulikuwa halali na mgombea wake Maalim Seif Sharif Hamad anafaa kutangazwa mshindi.

Mawaziri waliotoka chama cha CUF kwenye serikali iliyofaa kukamilisha muda wake mwanzoni mwa Novemba wamesema kisheria hawamo uongozini.

“Si kwamba tumejiuzulu lakini kisheria na kikatiba muda wetu wa kuhudumu ulimalizika Novemba 2,” amesema Nasor Abubakar Khamis Bakari, aliyekuwa waziri wa haki na masuala ya kikatiba.

“ZEC inafaa kutangaza CUF kuwa mshindi wa uchaguzi kwani hata katika majimbo tayari walitangaza washindi huko.”

Naibu katibu mkuu wa CUF Nassor Ahmed Mazrui, akihutubia kikao cha wanahabari mapema leo mjini Dar es Saaam amesema chama hicho hakijafurahishwa na shughuli inayoendelezwa kwa sasa na ZEC.

Image caption Wawakilishi hao wa CUF walikuwa wamebeba vyeti walivyopewa na ZEC

Wawakilishi wateule 27 wa CUF kutoka Zanzibar, walioandamana na baadhi ya viongozi wa chama hicho kwenye kikao cha leo, walisema si haki kwa ZEC kufuta ushindi wao kwa kuwa walishapewa vyeti vya ushindi.