Wanajeshi wawili wa Marekani wauawa Jordan

Jordan Haki miliki ya picha AFP
Image caption Marekani imekuwa ikitoa mafunzo kwa maafisa wa polisi wa Iraq na Palestina

Wanajeshi wawili wa Marekani na afisa mmoja wa Afrika Kusini wameuawa kwa kupigwa risasi katika kituo cha kutoa mafunzo kwa maafisa wa polisi nje ya mji mkuu wa Jordan, Amman, maafisa wa usalama wamesema.

Kituo hicho kinachofadhiliwa na Marekani katika mtaa wa Muwaqqar, viungani mwa mji wa Amman, hutumiwa kutoa mafunzo kwa maafisa wa polisi wa Iraq na Palestina.

Msemaji wa serikali ya Jordan Mohammad Momani amesema mshambuliaji huyo aliwajeruhi Wamarekani wengine wanne na Wajordan wanne kabla ya kuuawa na maafisa wa polisi wenzake.

Bw Momani ameambia shirika la habari la Petra kwamba kisa hicho kinachukuliwa uhalifu na kwamba uchunguzi umeanzishwa.

Afisa wa polisi aliyetekeleza mauaji hayo alikuwa mkufunzi wa ngazi ya juu wa cheo cha kapteni, afisa mmoja wa Jordan alinukuliwa na shirika la habari la Reuters.

Haijabainika ni nini kilichochochea shambulio hilo.

Ubalozi wa Marekani katika mji wa Amman uliandika kwenye Twitter kwamba umepokea habari kuhusu kicha hicho.

"Tunawasiliana na maafisa husika wa serikali ya Jordan, ambao wameahidi kusaidiana nasi kikamilifu."

Kisa hicho kimetokea wakati wa makumbusho ya miaka 10 tangu kutekelezwa kwa mashambulio ya mabomu na kundi la al-Qaeda katika hoteli tatu mjini Amman, shambulio lililoua watu 50.