Netanyahu aahidi kuendelea kutafuta amani

Netanyahu Obama Haki miliki ya picha AP
Image caption Israel inataka usaidizi zaidi kutoka kwa Marekani

Rais wa Marekani Barack Obama na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamesema wamejitolea kufanikisha amani Mashariki ya Kati.

Huo ulikuwa mkutano wao wa kwanza kabisa wa ana kwa ana tangu kudorora kwa uhusiano kati yao kutokana na kutiwa saini kwa mkataba wa nyuklia kati ya mataifa yenye ushawishi duniani na Iran.

Bw Netanyahu yumo ziarani Marekani ambako anatarajiwa kuomba kuongezwa kwa msaada wa kila mwaka wa kijeshi kwa Israel.

Kwenye hotuba fupi kabla ya mkutano huo White House, Bw Obama alisema atatafuta maoni kutoka kwa mwenzake kuhusu njia za kupunguza makabiliano kati ya Wapalestina na Waisraeli.

Alisema anataka makundi hayo mawili yarejee kwenye “njia ya kufikia amani”.

Bw Netanyahu alikariri msimamo huo kwa kusema, “hatujakata tamaa katika juhudi za kutafuta Amani”.

Alisisitiza hamu yake kuu ya kuwa na suluhu itakayopelekea kuwepo kwa mataifa mawili (taifa la Wayahudi na taifa la Wapalestina).

Viongozi hao pia wanatarajiwa kushauriana kuhusu mzozo unaoendelea sasa nchini Syria pamoja na utekelezajiwa mkataba wa nyuklia na Iran.