Zanzibar:Shein akutana na Maalim Seif

Image caption Rais wa Zanzibar Dokta Ali Mohammed Shein

Mazungumzo ya kutafuta suluhu ya mgogoro wa visiwani Zanzibar yameendelea huku mkutano uliowaleta pamoja rais Ali Mohammed Shein na kiongozi wa upinzani Seif Sharif Hamad ukifanyika.

Kulingana na gazeti la The Citizen nchini Tanzania, mkutano huo wa faragha katika ikulu ya rais ulihudhuriwa na marais wa zamani Ali Hassan Mwinyi na Amani Abeid karume.

Ni mara ya kwanza kwa Dkt Shein ambaye anatoka Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Bw Seif wa Chama cha Wananchi (CUF) ambaye ni makamu wa rais wa kisiwa hicho kukutana tangu tume ya uchaguzi kufutilia mbali matokeo ya urais.

Kushirikishwa kwa marais hao wa zamani ni thibitisho kwamba kuna harakati za kisiasa zinazoendelea katika juhudi za kukabiliana na tatizo hilo ambalo limezua mgogoro wa kikatiba.

Wanachama wa jumuiya ya kimataifa pia wanadaiwa kushiriki katika kumaliza tatizo hilo.

Hakuna habari zilizotolewa kutoka pande zote mbili lakini duru za serikali zimethibitisha kwamba mazungumzo hayo yalifanyika kwa faragha.

Image caption Maalim Seif Hamad wa Zanzibar

Makamu wa rais wa pili Seif Ali Idd pia amedaiwa kuhudhuria mkutano huo kulingana na duru hizo.

Bw Mwinyi alikuwa rais wa Zanzibar kwa kipindi kifupi kabla ya kuteuliwa kuwania urais mwaka 1985 huku Karume akiliongoza eneo hilo kutoka mwaka 2000 hadi mwaka 2010.

Maafisa wa ikulu ya rais visiwani Zanzibar hawakuwa tayari kuzungumzia kuhusu yalioafikiwa katika mkutano huo.

Wale kutoka CUF hata hivyo wamesema kuwa majadiliano yalikuwa mazuri kwa maslahi ya raia wa muungano wa Tanzania.