Afrika na Ulaya kuukabili uhamiaji

Wahamiaji Haki miliki ya picha AFP
Image caption Maelfu ya Waafrika wamekuwa wakikimbilia Ulaya kutoroka hali ngumu ya maisha

Viongozi wa Ulaya na Afrika wameanza mkutano wao unaolenga kutafuta njia za kuzuia wimbi la wakimbizi wa Kiafrika wanaoelekea Ulaya.

Tume ya Umoja ya Ulaya imetoa kiasi cha karibu dola bilioni mbili zitakazo saidia kampeni za kuhamasisha watu kuachana na safari za kuelekea Ulaya hususan kwa kutumia njia ya bahari.

Aidha Viongozi wa Afrika katika mazungumzo hayo ya Malta wamesisitiza kwamba Ulaya ni lazima ijiandae kushirikiana, kuliko kutafuta ufumbuzi kwa kutoa masharti tu.

Mkutano huu wa Malta uliandaliwa kufuatia mfululizo wa matukio ya vifo baada ya meli zilizobeba wahamiaji kuzama katika maeneo ya Afrika kaskazini na kabla ya wimbi la hivi karibuni la wahamiaji wanaoingia barani Ulaya kupitia Uturuki na Ugiriki.

Kwa upande wake, Rais wa Senegal Macky Sall ametaka kuwepo kwa huduma iliyo sawa kwa wahamiaji bila ya kujali utaifa wa mhamiaji.

Naye Mkuu wa Sera za Nje wa Umoja wa Ulaya Federica Mogherini amesema umoja huo hautatoa fedha tu, lakini pia kujenga fursa kwa watu, kulinda maisha ya watu, kupambana na mitandao ya kihalifu. '