EU kutoa mabilioni kwa Afrika kupunguza wahamiaji

Wahamiaji Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Wahamiaji wengi wamekuwa wakifa maji wakijaribu kufika Ulaya

Viongozi wa Muungano wa Ulaya wanatarajiwa kutoa mabilioni ya euro kwa mataifa ya Afrika kuyawezesha kusaidia kupunguza mzozo wa wahamiaji Ulaya.

Tume ya Muungano wa Ulaya imesema itatoa €1.8bn (£1.3bn) na inatarajia mataifa zaidi ya EU yaahidi pesa zaidi.

Lengo la ufadhili huo ni kusaidia kusuluhisha matatizo ya kiuchumi na kiusalama ambayo huwafanya watu kutoroka mataifa ya Afrika. Aidha, zitatumiwa kuyashawishi mataifa ya Afrika kuwapokea watu ambao wamenyimwa hifadhi Ulaya.

Ahadi hiyo inatarajiwa kutolewa kwenye mkutano mkuu kuhusu wahamiaji unaofanyika Malta, na ambao ulipangwa baada ya meli iliyobeba wahamiaji kuzama Libya mwezi Aprili. Watu 800 walifariki

Watu 150,000 wamevuka bahari ya Mediterranean kutoka Afrika mwaka huu, wengi wakitua Italia na Malta.

Hata hivyo, mtazamo wa EU umebadilika tangu Aprili na kuangazia zaidi wakimbizi wanaotoka mashariki na hasa Syria, ambao wanawasili kwanza Ugiriki na kuvuka hadi Uturuki kisha kuelekea kaskazini kupitia bataifa ya Balkan.

Zaidi ya viongozi 60 kutoka Afrika na Ulaya, akiwemo Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, wanakutana Valletta, Malta kwa mkutano huo mkuu wa siku mbili kujadili uhamiaji.

Tume ya Muungano wa Ulaya itaweka pesa hizo €1.8bn kwenye "hazina maalum" kwa ajili ya Afrika na imehimiza mataifa wanachama kufikisha kiasi hicho cha pesa.

Hata hivyo, kuna shaka kuhusu iwapo mataifa hayo yatakubali wito huo.