Maandamano Nigeria kutetea 'mtetezi' wa Biafra

Kanu
Image caption Waigbo wengi wanahisi serikali kuu haijali maslahi yao

Mamia ya watu kusini mwa Nigeria wameandamana kushinikiza kuachiliwa huru kwa mwanaharakati anayetetea kujitenga kwa jimbo la Biafra.

Mkurugenzi huyo wa kituo cha redio cha Radio Biafra, ambacho kimepigwa marufuku, Bw Nnamdi Kanu, alikamatwa mwezi uliopita na bado anazuiliwa na polisi licha ya mahakama kuagiza aachiliwe huru.

Kumekuwepo na ripoti za kuzuka kwa fujo wakati wa maandamano katika mji wa Port Harcourt.

Waliokuwa wakipigania kujitenga kwa Biafra walipigana vita vikali miaka mitatu ambavyo vilimalizika 1970.

Watu zaidi ya milioni moja waliuawa kabla ya maasi hayo kuzimwa na jeshi.

Makundi yanayotaka kujitenga kwa eneo hilo, hasa kutoka jamii ya Waigbo, yamekuwa yakivutia vijana wengi miaka ya hivi karibuni.

Mwandishi wa BBC Abdussalam Ahmed katika mji wa kusini mashariki wa Enugu anasema wengi hawataki kujirudia kwa mapigano ya wenyewe kwa wenyewe lakini sana wanataka serikali iangazie matatizo yanayokumba eneo hilo.

Image caption Kanu amezuiliwa kwa zaidi ya wiki tatu

Wanaharakati wameambia BBC kwamba watu watano waliuawa na wengine kadha kujeruhiwa baada ya polisi kufyatulia risasi waandamanaji katika mji wa Port Harcourt ulio mkubwa eneo hilo.

Lakini msemaji wa polisi Ahmad Muhammad amekanusha habari hizo.