Mchezaji achunguzwa kwa kuchokoza mbwa

Oakland Haki miliki ya picha Getty
Image caption Klabu ya mchezaji huyo ilishindwa kwenye mechi hiyo

Mchezaji wa Oakland Raiders Ray-Ray Armstrong anachunguzwa na maafisa wa polisi kwa tuhuma za ‘kubweka’ na kujipiga kifua mbele ya mbwa wa polisi.

Armstrong, 24, anadaiwa kuinua shati lake na kumchokoza mbwa huyo kabla ya mechi ya NFL dhidi ya Pittsburgh Steelers Jumapili.

Akipatikana na hatia, huenda akashtakiwa na kosa la kumchokoza mbwa wa polisi, ambalo ni kosa la ngazi ya tatu jimbo la Pennsylvania.

"Mbwa huyo alijawa na hasira sana,” afisa mmoja wa polisi Kevin Kraus amesema.

"Afisa huyo alitatizika sana kumdhibiti mbwa huyo. Tulifahamishwa mara moja kuhusu kisa hicho na mara moja tukaanzisha uchunguzi.”

Afisa wa polisi aliyekuwa na mbwa huyo, Bi Maria Watts, amemtambua Armstrong kuwa ndiye aliyehusika katika kisa hicho.

Ameambia runinga ya WTAE Pittsburgh kwamba maafisa wa polisi wamekasirishwa sana na kisa hicho.

Klabu zote mbili zimejulishwa kuhusu tukio hilo na NFL imeanzisha uchunguzi.

Oakland Raiders walilazwa 38-35 na Steelers.