Aliyeruhusiwa kutazama Star Wars mapema afariki

Image caption Mwezi Julai, daktari alikuwa amesema Fleetwood angeishi miezi miwili pekee zaidi

Daniel Fleetwood, shabiki aliyeruhusiwa kutazama filamu mpya ya Star Wars ya The Force Awakens mapema, amefariki akiwa na umri wa miaka 32.

Mkewe Ashley aliandika habari za kifo chake kwenye mtandao wa Facebook.

Aliandika: “Daniel alipigana vita hadi mwisho. Sasa ameenda kwa Mungu. Alifariki akiwa usingizini. Atakuwa shujaa wangu daima.”

Waigizaji nyota wakiwemo Mark Hamill walikuwa wameungana na kusaidia kampeni ya kushinikiza Disney imruhusu Daniel atazame filamu hiyo mpya, ambayo itaonyeshwa mara ya kwanza mwezi ujao.

Bw Fleetwood, alikuwa anaugua saratani na aliambiwa na madaktari mwezi Julai kwamba alikuwa amesalia na miezi miwili pekee ya kuishi.

Alipewa fursa ya kutazama filamu hiyo baada ya kampeni iliyoendeshwa katika mitandao ya kijamii ikiwa na kitambulisha mada #ForceForDaniel, ambapo raia walitoa wito kwa waandalizi wa filamu hiyo wamruhusu kuitazama filamu hiyo mapema.