Ndege za Misri zapigwa marufuku Urusi

Egypt Air Haki miliki ya picha AFP
Image caption Ndege za Egypt Air ndizo pekee zilikuwa zinahudumu kati ya Misri na Urusi

Mamlaka ya safari za ndege nchini Urusi imepiga marufuku ndege za shirika la taifa la ndege la Misri kuhudumu Urusi, msemaji wa uwanja wa ndege Moscow amesema.

Safari za ndege kutoka Urusi hadi Misri tayari zilikuwa zimesimamishwa baada ya ndege ya Urusi kuanguka eneo la Sinai mwezi jana.

Abiria wote 224 walifariki, wengi wao wakiwa raia wa Urusi.

Shirika hilo la Egypt Air ndilo pekee lililokuwa limesalia likifanya safari kati ya mataifa hayo mawili.

Haki miliki ya picha EPA

Vyombo ya habari Urusi zinasema shirika hilo limepigwa marufuku kuhakikisha linatimiza matakwa ya kiusalama.

Kundi la Sinai Province, lenye ushirika na Islamic State, limedai kuhusika katika kuangusha ndege ya Metrojet nambari 9268, iliyokuwa ikitoka Sharm el-Sheikh kuelekea St Petersburg Urusi.

Mataifa ya Magharibi yamesema kuna uwezekano mkubwa bomu lililipuka ndani ya ndege hiyo ikiwa angani, lakini Urusi na Misri zimesema ni mapema mno kuthibitisha hayo.

Baada ya ajali hiyo, mataifa kadha, ikiwemo Uingereza, yalisitisha safari za ndege za kuingia na kutoka Sharm el-Sheikh, yakitaja wasiwasi kuhusu usalama.