Kiongozi wa upinzani amekamatwa Niger

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Hama Amadou,ni waziri mkuu wa zamani wa Niger

Kiongozi wa upinzani huko Niger amekamatwa aliporudi nchini humo mwaka mmoja baada ya kutoroka akiwa anakabiliwa na mashtaka ya biashara ya ulanguzi wa watoto.

Hama Amadou,ambae ni waziri mkuu wa zamani wa Niger amezuiliwa katika uwanja wa ndege wa Niamey .

Watu wengine 30 akiwemo mkewe Amadou pia wamekuwa wakizuiliwa kwa mashtaka ya kutumia njia zisizo za kisheria kuwapata watoto wachanga na kisha kuwauzia matajiri wa huko Niger.

Amadou na wahusika hao wengine wamekana madai hayo wakisema ni mbinu ya ukandamizwaji wa kisiasa.

Mapema polisi waliwafyatulia mabomu ya kutoa machozi wafuasi wa Amadou waliokuwa wanapinga kukamatwa kwake .

Mwezi juzi Amadou alikuwa ametangaza kuwa atarudi nchini humo kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwaka ujao.