Watu 4 wameuawa usiku wa jana Bujumbura

Image caption Polisi wamethibitisha kuwa afisa mmoja wa polisi alipoteza maisha yao huku watu wengine watatu wakipatikana wamekufa karibu na jumba la burudani katika kitongoji cha Bwiza.

Mauaji yameendelea kuripotiwa katika mji mkuu wa Burundi Bujumbura.

Polisi wamesema watu wanne wameuawa usiku wa jana katika mashambulio yaliyotokea maeneo tofauti ya mji mkuu.

Milio ya gruneti aidha imesikika usiku wa kuamkia leo.

Hii ni licha ya operesheni ya kutwaa silaha haramu inayoendeshwa na serikali ya rais Nkurunziza

Machafuko nchini humo yameendelea tangu rais Pierre Nkurunziza kuamua kuwania muhula wa tatu uliozua utata wa kisiasa.

Haki miliki ya picha
Image caption Mauaji yameendelea kuripotiwa katika mji mkuu wa Burundi Bujumbura.

Watu wengine wengi wamejeruhiwa kufuatia mashambulizi hayo yaliyotapakaa kote mjini Bujumbura.

Mashambulizi zaidi ya guruneti yaliendelea hadi mapema leo.

Moja ya majumba yaliyolengwa katika mashambulizi hayo ni ile inayomilikiwa na meya wa mji wa Bujumbura.

Mke wake aliiambia BBC kuwa ''Ni muujiza kuwa hakuna aliyepoteza maisha yake ndani ya nyumba hiyo''

Nyumba ya Freddy Mbonimpa pia iliharibiwa katika mashambulizi hayo.

'Ajabu ni kuwa bomu moja lilipenyeza ndani ya chumba cha kulala cha watoto ila halikulipuka''Aliambia mwandishi wa BBC.

Haki miliki ya picha AFP
Image caption Zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha yao huku wengine laki mbili wakihamia mataifa jirani.

Mashambulizi hayo yalitokea katika eneo la Rohero ambalo halikuwa limeathirika sana na machafuko ya kisiasa yaliyoanza tangu mwezi Aprili.

Polisi wamethibitisha kuwa afisa mmoja wa polisi alipoteza maisha yao huku watu wengine watatu wakipatikana wamekufa karibu na jumba la burudani katika kitongoji cha Bwiza.

Watu wapatao 12 wanauguza majeraha.

Ni juma moja tangu serikali iliposema kuwa itatumia mitambo ya kisasa kutambua kulikofichwa silaha ila sasa inaonekana tatizo ni kubwa kuliko ilivyokuwa imetarajiwa.

Jumuia ya mataifa imekuwa ikishawishi serikali ya rais Nkurunziza kufanya mazungumzo ya amani na wapinzani wake ilikutafuta suluhu ya mzozo huo wa kisiasa.

Hadi kufikia sasa zaidi ya watu 200 wamepoteza maisha yao huku wengine laki mbili wakihamia mataifa jirani.