Watu 32 wauawa kaskazini mwa Nigeria

Yola
Image caption Mji huo umeshambuliwa mara kwa mara mwaka huu

Watu 32 wameuawa kwenye shambulio la bomu la kujitoa mhanga katika mji wa Yola, kaskazini mashariki mwa Nigeria. Wengine 80 wamejeruhiwa.

Maafisa wa huduma za dharura wanasema miili ya waliofariki imepelekwa vyumba vya kuhifadhia maiti huku waliojeruhiwa wakipelekwa hospitalini.

Baadhi ya majeruhi walikuwa wamevunjika miguu na mikono.

Walioshuhudia shambulio hilo wanasema lilikuwa kubwa kiasi kwamba mlipuko ulisikika kote jijini.

Shambulio hilo lilitokea karibu na soko la mboga majira ya jioni.

Mji wa Yola umekuwa ukishambuliwa mara kwa mara, anasema mwandishi wa BBC aliye Abuja Abdullahi Kaura Abubakar.

Mji huo umeshuhudia milipuko miwili ya mabomu iliyoua watu zaidi ya hamsini mwaka huu na mojawapo wa miji iliyoathirika na mashambulio ya wapiganaji wa Kiislamu wa Boko Haram.