Moja kwa Moja: Operesheni Saint Denis

Boya hapa kwa habari za karibuni zaidi

14:32 Disneyland watangaza kwamba watafungua vituo vyao vya burudani mjini Paris kesho.

14:30 Waziri wa masuala ya ndani wa Ufaransa Bernard Cazeneuve azuru eneo la Saint Denis na kuwasifu maafisa wa usalama kwa ujasiri wao.

Haki miliki ya picha Getty

14:20 Msemaji wa serikali ya Ufaransa asema operesheni Saint Denis imemalizika. Watu saba walikamatwa kwenye operesheni hiyo. Mtu mmoja, mwanamke aliyejilipua, alifariki. Mwanamke huyo anadaiwa kuwa jamaa wa mshukiwa mkuu wa mashambulio ya Novemba 13 Abdelhamid Abaaoud. Mbwa wa polisi kwa jina Diesel pia ameuawa.

13:20 Eneo ambalo polisi wameshambulia mtaa wa Saint Denis ni karibu na uwanja wa taifa wa Stade de France ambako milipuko ilitokea Novemba 13.

13:00 Mwanamume akamatwa na maafisa wa usalama eneo lililoshambuliwa mtaa wa Saint Denis.

Haki miliki ya picha EPA

12:25 Maafisa watano wa polisi wamepata majeraha 'madogo' wakati wa operesheni Saint Denis, mhariri wa BBC wa Ulaya Katya Adler ameandika kwenye Twitter.

12:05 Mbwa wa polisi ameuawa kwenye makabiliano Saint Denis, kituo cha televisheni cha BFMTV kimeripoti.

Haki miliki ya picha AFP

11:40 Polisi waliovalia barakoa wanaripotiwa kuingia ukumbi wa baraza la manispaa wa Saint Denis. Ripoti zinasema bado kuna mtu mmoja aliyejifungia ndani ya nyumba iliyoshambuliwa na polisi mtaa huo.

Haki miliki ya picha AFP

11:03 Duru zinasema mwanamgambo wa Islamic State Abdelhamid Abaaoud, ambaye awali alidaiwa kupanga mashambulio hayo ya Paris Ijumaa iliyopita akiwa Syria, ndiye aliyekuwa akisakwa na maafisa wa usalama kwenye nyumba moja mtaa wa St Denis. Mashambulio hayo katika maeneo sita Novemba 13 yalisababisha vifo vya watu 129.

10:55 Bado kuna utata kuhusu idadi ya wanamgambo waliouawa kwenye operesheni ya vikosi vya usalama St Denis baadhi ya ripoti zikisema wawili na nyingine watatu.

10:50 Wakazi wa mtaa wa St Denis wanachunguzwa kwa makini na maafisa wa usalama huku operesheni eneo hilo ikiendelea. Eneo hilo limezingirwa na wanajeshi. Maduka na shule zimefungwa. Huduma za uchukuzi pia zimesitishwa.

10:25 Watu watatu wamekamatwa kwenye operesheni ya pamoja ya wanajeshi na maafisa wa polisi mtaa wa Saint Denis, duru za polisi zaambia shirika la habari la AFP.

Haki miliki ya picha AP

10:15 Watu watatu wameuawa kwenye operesheni ya polisi mtaa wa Saint Denis, kaskazini mwa mji wa Paris. Mionogni mwa waliouawa, kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, ni mwanamke aliyejilipua. Maafisa watatu wa polisi wamejeruhiwa kwenye operesheni hiyo.

10:08 Polisi wanukuliwa na shirika la AP wakisema wanaamini mhusika mkuu kwenye mashambulio ya Ijumaa Abdelhamid Abaaoud, amejifungia kwenye nyumba inayoshambuliwa Saint Denis, pamoja na watu wengine watano wenye silaha.

Haki miliki ya picha Reuters

09:55 Shirika la habari la AP linasema kumetokea milipuko saba kwenye eneo la makabiliano kati ya polisi na watu wenye silaya mtaa wa Saint Denis asubuhi.

09:50 Mbunge mmoja Mathieu Hanotin aambia kituo cha redio cha France Inter Radio kwamba operesheni bado inaendelea. "Watu wasitoke nje. Watu wenye silaha bado wamejifungia ndani ya nyumba."

09:40 Mkazi mmoja wa Saint Denis amesimulia shirika la AP jinsi mambo yalivyoanza mtaani huo.Baptiste Marie, 26, ambaye ni mwanahabari anayeishi karibu na eneo ambako ufyatulianaji wa risasi umetokea amesema: "Tulianza kusikia mlipuko. Kisha kukawa na mlipuko mwingine wa pili mkubwa. Na milipuko mingine miwili ikafuata. Kisha, ufyatulianaji wa risasi uliodumu saa moja."

09:35 Gazeti la Le Monde linaripoti kuwa watu wawili wameuawa kwenye operesheni hiyo, likinukuu duru za polisi.

09:30 Shirika la habari la AFP lasema mtu mmoja amefariki wakati wa operesheni ya polisi mtaa wa Saint Denis.

09:20 Polisi wamewaondoa raia kutoka eneo la ufyatulianaji wa risasi

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Raia wakiondoka eneo la ufyatulianaji wa risasi

09:15 Shirika la habari la AFP lanasema Abaaoud Abdelhamid, anayedaiwa kupanga mashambulio hayo, ndiye aliyekuwa akisakwa kwenye operesheni hiyo mtaa wa Saint Denis.

09:15 Naibu meya Stephane Peu amewahimiza raia wasalie manyumbani, akisema "hili si shambulio jipya bali ni operesheni ya polisi".

Haki miliki ya picha AP
Image caption Ufyatulianaji mkali wa risasi umesikika katika mtaa huo.

09:00 Maafisa wa polisi nchini Ufaransa wamefanya operesheni kali mtaa wa Saint Denis vingani mwa mji wa Paris ambao inadaiwa kulenga mhusika mkuu wa mashambulio yaliyotekelezwa Ijumaa.