Mamaake Samson Siasia atekwa nyara Nigeria

Image caption Aliyekuwa mchezaji soka wa timu ya Nigeria samson Siasia

Wapiganaji wamemteka nyara mamaake aliyekuwa mchezaji wa Nigeria Samson Siasa.

Watekaji nyara 3 walimteka Ogere Siasia kutoka nyumba ya familia hiyo katika jimbo la Bayelsa katika eneo lenye mafuta mengi la Niger Delta.

Mwanawe ameomba kuwachiliwa huru kwa mamaake huku akisema kwamba lengo la wapiganaji hao halijulikani.

Mwandishi wa BBC Chris Ewokor aliye katika mji mkuu wa Abuja,anasema kuwa utekaji nyara wa kulipa fidia hufanyika sana katika maeneo mengi ya Nigeria huku familia za wachezaji soka zikilengwa.

Mchezaji wa kimataifa wa Nigeria Christian Obodo alitekwa nyara katika eneo la Warri,kusini mwa Nigeria mnamo mwezi Juni 2012.

Mwaka mmoja kabla ya tukio hilo,babaake mchezaji wa Chelsea John Obi Mikel alitekwa nyara katika mji wa Jos katikati mwa Nigeria.

''Ninawaomba kumrejesha bila kumdhuru.Niliarifiwa kwamba walipiga risasi kadhaa hewani kabla ya kumchukua kwa pikipiki'',Samson aliiambia BBC.

''Hatujasikia habari zozote kutoka kwao ili kujua lengo lao,lakini kwa sasa nina wasiwasi kuhusu usalama wake''.aliongezea.