Vazi la Burqa kupigwa marufuku Senegal

Haki miliki ya picha Getty
Image caption Vazi la Burqa

Senegal inapanga kupiga marufuku uvaaji wa vazi la wanawake la Burqa kwa lengo la kuzuia mienendo ya makundi ya kijihadi,waziri wa maswala ya ndani nchini humo Abdoulaye Daouda amesema.

Waziri huyo amesema kuwa hatua hiyo haifai kuonekana kama inakiuka uislamu kwa kuwa taifa hilo lina waislamu wengi.

Iwapo mipango hiyo itakuwa sheria,Senegal litakuwa taifa la tano Afrika kupiga marufuku uvaaji wa vazi hilo.

Wiki iliopita ,rais wake Macky Sall,muislamu, alitangaza vita dhidi ya wapiganaji wa kiislamu.

Haki miliki ya picha Reuters
Image caption Rais Macky Sall wa Senegal

Chad,Gabon na Congo Brazzaville yametangaza marufuku kama hiyo ,huku Cameroon ikianzisha hatua hiyo mwezi Julai katika jimbo lake la Kaskazini.

Mataifa yote hayo yalikuwa chini ya ukolini wa Ufaransa,ambayo ilizua hisia kali mwaka 2011 ilipokuwa nchi ya kwanza barani Ulaya kupiga marufuku uvaaji wa vazi hilo katika maeneo ya uma .

Mataifa ya Chad na Cameroon yamelengwa na washambuliaji wa kujitolea muhanga ,wanaohusishwa na wapiganaji wa Boko Haram kutoka Nigeria,ambao wapiganaji wake mara nyengine huvaa vazi la kujifunika uso ili kuingia katika maeneo yenye watu wengi.